Kikosi cha Simba kuanza safari kuelekea Mbeya kuifuata Ihefu FC
KIKOSI cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji, leo Septemba Mosi kinatarajiwa kuanza safari kuelekea Mbeya kuifuata Ihefu FC. Simba iliweka ngome mkoani Arusha tangu Agosti 28 ambapo ilitia timu siku ya Ijumaa kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 30,Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Kwenye mchezo huo ambao ni maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, Simba ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa ba John Bocco dk ya 7 na Bernard Morrison dk ya 60. Wanaanza safari ya kutetea taji la Ligi Kuu Bara kwa kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Ihefu Septemba 6 Uwanja wa Sokoine majira ya saa 10:00 jioni. Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa timu zote ndani ya msimu mpya wa 2020/21 huku Ihefu ikiwa ni msimu wake wa kwanza pia kushiriki Ligi Kuu Bara baada ya kupanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza.