Rais wa Lebanon akiri haja ya "kuubadili mfumo"
Rais wa Lebanon Michel Aoun amekiri haja ya "kuubadilisha mfumo" wa kisiasa nchini humo na kutoa wito wa kutangazwa taifa lisiloegemea dini katika mkesha wa ziara ya mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Mshirika wa kisiasa wa Aoun, mkuu wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah pia alisema mapema kuwa anakaribisha pendekezo la Macron la kuwepo mkataba mpya wa kisiasa Lebanon.
Wakati huo huo vigogo wa kisiasa wa madhehebu ya Sunni akiwemo waziri mkuu wa zamani Saad Hariri wamempendekeza Mustapha Adib kuwa waziri mkuu mpya, hatua ambayo vuguvugu la maandamano Lebanon liliipinga mara moja likisema inakwenda kinyume na mabadiliko wanayoyataka.
Adib, mwenye umri wa miaka 48, ni balozi wa Lebanon nchini Ujerumani na hafahamiki sana katika ulingo wa kisiasa.
Ikiwa chini ya wiki nne baada ya kuzuru Beirut kufuatia mlipuko mkubwa katika bandari ya mji huo uliowauwa zaidi ya watu 180, Macron anarejea nchini humo leo kushinikiza masharti yake ya kufanywa mabadiliko.
Comments
Post a Comment