Rwanda yaitaka Ufaransa kumkamata mshukiwa wa mauaji ya kimbari
Rwanda imeitaka Ufaransa kumkamata Aloys Niwiragabo anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Mtuhumiwa huyo alikuwa kanali wa jeshi, aliyehusika na upelelezi katika enzi za utawala wa hayati Juvenal Habyarimana.
Mwendesha mashitaka mkuu wa Rwanda Aimable Havugiyaremye ametangaza kwamba Rwanda tayari imetoa waranti wa kutaka Kanali Aloys Ntiwiragabo akamatwe.
‘’Kwa sasa tunafanya kazi kwa ushirikiano na kundi la wapelelezi wa makosa ya uhalifu wa kivita nchini Ufaransa.Wapepelezi hao tayari wameishaanza uchunguzi wao na kazi inaenda kama ilivyopangwa.’’
Kwa mjibu wa mwendesha mashtaka mkuu wa Rwanda Bw. Ntiwiragabo, anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari japo hakutoa maelezo zaidi.
Kanali Aloys Ntiwiragabo mwenye umri wa miaka 72 alikuwa mkuu wa idara ya upelelezi wa jeshi wakati wa utawala wa hayati Juvenal Habyarimana.
Kanali huyo alikuwa miongoni mwa maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi la hayati Juvenal Habyarimana, lakini hayupo kwenye orodha ya watuhumiwa wakuu wa mauaji ya kimbari ambao bado wanasakwa na mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda.
Wengine waliopo kwenye orodha hiyo ni Protais Mpiranya aliyekuwa kamanda wa kikosi cha ulinzi wa Habyarimana na Augustin Bizimana aliyekuwa waziri wa ulinzi lakini yeye imethibitishwa kufariki nchini Congo Brazaville.
Waranti wa kumkamata mtuhumiwa huyo umetolewa ukifwatia kukamatwa kwa mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya kimbari Felicien Kabuga aliyekamatwa nchini Ufaransa mwezi Marchi baada ya kujificha kwa miaka 26.
Comments
Post a Comment