Ujerumani yaondowa vikwazo vya safari ilivyoweka kwa COVID-19
Hatimaye Ujerumani imeondosha marufuku yake ya safari kwa nchi zote ambazo hazipo kwenye Umoja wa Ulaya, huku kila dalili zikionesha kuwa wimbi jipya la maambukizo ya virusi vya corona linaanza tena barani Ulaya. Kufunguliwa huko upya kwa mipaka na viwanja vya ndege kuliamuliwa na baraza la mawaziri wiki tatu zilizopita, lakini utekelezaji wake umeanza Alkhamis ya leo. Mataifa 160 duniani yanafaidika na uamuzi huu. Hata hivyo, uamuzi huu unaanza kutekelezwa wakati idadi ya maambukizo mapya ya COVID-19 ikipanda barani Ulaya, huku wengi wakionya kwamba bara hili limo kwenye ukingo wa kutumbukia kwenye awamu ya pili ya janga la virusi vya corona. Ujerumani ilitowa indhari ya safari kwa ulimwengu mzima mnamo mwezi Machi, wakati virusi hivyo vikisambaa kwa kasi kaskazini mwa Italia, lakini ikaiondosha kwa mataifa mengi ya Ulaya mwezi Juni. Mwezi uliopita, Ujerumani ilianza tena kutangaza tahadhari kwa maeneo kadhaa ya Ulaya, baada ya maambukizo kuanza tena kupanda kw...