Ditopile azidi kuibomoa CHADEMA, Awarudisha wanachama wao 26 CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kata
Amsha amsha ya Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile kwenye uzinduzi wa kampeni za Udiwani Kata ya Mpamantwa wilayani Bahi zimefanikiwa kuwarudisha kwenye chama hicho wanachama 26 wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kata hiyo, Emmanuel Elias.
Akizungumza katika uzinduzi huo ambao amemnadi Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, Mgombea Ubunge Kenneth Nolo na Mgombea Udiwani Sosthenes Mpandu amesema Rais Magufuli mwaka 2015 alisema anataka kwenda kushughulika na shida za wananchi na kweli ametekeleza ahadi yake hiyo ambapo leo elimu ya msingi hadi kidato cha nne ni bila malipo wazazi hawalipi badala yake Serikali ya Dk Magufuli inalipa zaidi ya Sh Bilioni 24 kila mwezi ili watoto wakasome.
" Magufuli alisema anaenda kujenga Hospitali kila Halmashauri au Wilaya, kwenye Hospitali zaidi ya 70 zilizojengwa Nchi nzima nyie watu wa Bahi mna Hospitali ambayo Dk Magufuli ameijenga kwa Sh Bilioni 1.7 sambamba na vifaa tiba vyake, amejenga vituo 484 Nchi nzima, hapa Bahi vimejengwa vituo vya afya vinne, ametupendelea sana twendeni tukampe kura nyingi za heshima hadi wapinzani wakome kugombea nae.
Hapa Bahi yenyewe miaka saba nyuma haikua Wilaya leo tumekua Wilaya tuna Mkuu wa Wilaya na Halmashauri, Hospitali, Vituo vya Afya vya kutosha hivyo hatusafiri tena umbali mrefu kwenda kutatuliwa shida zetu maana DC na Mkurugenzi wapo hapa, changamoto za kiafya zinamalizwa hapa, Mji umekua na fursa za maendeleo zimepanuka," Amesema Ditopile.
Amewaomba wananchi wa Bahi kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 kwenda kuipigia kura CCM ili iweze kuwatumikia kwa miaka mingine mitano na kuachana na maneno ya wapinzani ambao hata ilani yao inaonesha waichukua nchi wataweka rasilimali za watanzania rehani.
Comments
Post a Comment