Mama Samia ahitimisha ziara mkoani Manyara, aahidi kutatua Changamoto za Maji na Umeme


Na John Walter-Hanang

Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama cha Mapinduzi Samia Hassan amesema endapo Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuongoza katika miaka Mitano ijayo, watahakikisha changamoto zote za Maji na umeme zinamalizika.

Samia Hassan ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  ametoa ahadi hizo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Hanang mkoani Manyara Septemba 30, 2020 katika kampeni za Chama hicho za kunadi ilani ya mwaka 2020-2025 iliyofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Katesh A.

Amesema serikali ya Ccm chini ya uongozi wa Rais John  Pombe Magufuli inayojali wanyonge itahakikisha suala la tatizo la Maji, Umeme na Miundo mbinu ya bara bara linamalizika  nchini.

"Kwa hiyo mniamini kwamba maeneo yote ambayo hayana maji, maji yanakuja" alisema Samia.

Ameongeza kuwa serikali ya Chama cha Mapinduzi  inakwenda kuifanyia kazi ahadi ya  kuweka kituo cha Afya kila kata na Zahanati kila kijiji ili kuwasogezea wananchi huduma karibu huku utaratibu wa Elimu bila malipo ukiendelea kama ulivyokuwa katika kipindi cha miaka mitano inayomalizika, kuboresha na kujenga miundo mbinu ya Elimu pamoja kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Samia amewaomba wananchi ifikapo Oktoba 28 mwaka huu kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura na kuchagua viongozi wa chama Chama Mapinduzi ili waweze kutimiza ahadi zote walizozitoa za kuleta Maendeleo.

Mgombea Ubunge Jimbo la Hanang Mhandisi Samwel Hayyuma amesema serikali imejenga Zahanati katika Jimbo hilo ila kwa kuwa Jimbo ni kubwa amemuomba Makamu wa Rais kumweleza Rais Magufuli kwamba, Jimbo hilo linahitaji kupatiwa Vituo vya afya na zahanati katika kata na vijiji vingine pamoja na bara bara ya lami kilomita 10.

 Amesema Jimbo hilo litabaki kuwa la kijani na kwamba hakuna mpinzani anaeweza kupata hata kata moja.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake katika mkoa wa Manyara ya kunadi sera za Chama cha Mapinduzi akieleza mambo yaliyofanyika katika kipindi cha Miaka Mitano inayomalizika na yatakayofanyika kwa kipindi kingine kijacho endapo watapata ridhaa ya kuendelea kuongoza wananchi.

Mama Samia Oktoba mosi  anatarajia kuanza Ziara ya Kampeni katika mkoa wa Singida.



Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato