Jamshid bin Abdullah Al Said: Fahamu aliko Sultani wa mwisho wa Zanzibar

 


Baada ya kuishi mafichoni hususan nchini Uingereza Jamshid bin Abdullah Al Said, aliyekuwa sultani wa Zanzibar , akiwa ndio Sultan wa mwisho wa mssultani waliotawala miaka 91 kisiwani humo kutoka kwa familia ya al Busaid , alihamia katika ufalme wa Oman.


Mtu huyu ambaye aliitawala Zanzibar hadi alipoondolewa katika mapinduzi ya mwezi Januari 1964 aliwasili mjini Muscat hivi karibuni.


Gazeti la The Guardian linasema kwamba serikali ya Oman ilikataa maombi kadhaa yaliotolewa na Sultan huyo ili kumruhusu kuishi katika ufalme huo.


Lakini ndugu yake mmoja mjini Muscat aliambia gazeti la The National mjini Abu Dhabi kwamba ombi lake la kutaka kuishi Oman limekubalika kutokana na umri wake.


Amekua akitaka kuishi siku zake za mwisho katika taifa hilo la mababau zake ''na sasa anafurahia kuweza kufanya hivyo'', aliongezea.


Afisa mmoja wa serikali alikataa kutoa tamko lake kulingana na gazeti la The Guardian.


Uhuru na mapinduzi


Jamshid bin Abdullah alizaliwa tarehe 16 Septemba 1929 na kuwa Sultan wa Zanzibar baada ya kifo cha babake , Abdullah Bin Khalifa mwezi Julai 1963.


Mnamo mwezi Disemba 1963, kisiwa hicho kilichopo maili 22 kutoka kwa pwani ya Tanzania kilijipatia Uhuru wake kutoka kwa Uingereza.



Ijapokuwa kuna madai kwamba mapinduzi hayo yaliwahusisha wapaiganaji 600 chini ya uongozi wa kikomunisti wa John Okelo, yaliungwa mkono na raia wengi wa Afrika.


Maelfu ya Waarabu waliuawa katika ghasia huku maelfu zaidi wakitoroka visiwa hivyo kwa hofu ya maisha yao.


Baada ya kuangushwa kwa usultani mwezi januari visiwa vya zanzibar vikawa Jamhuri. mwezi Aprili rais wa Zanzibar na Tanganyika walitia saini ya kuwa na taifa moja kwa jina Tanzania, ambapo Zanzibar ilibaki na sehemu ya uhuru wake.


Uhamishoni

Jamshid bin Abdullah alitoroka Zanzibar kwa kutumia dau moja la kifahari baada ya wanamapinduzi kuliteka kasri lake.


Baada ya kukataliwa kuingia Oman, alisafiri hadi Uingereza akiwa na ndugu na jamaa zake . Wiki mbili baadaye Gazeti la The New York Times liliripoti kwamba hali ya kifedha ya Sultan huyo ilimlazimu kuondoka katika hoteli ya kifahari aliokuwa akiishi karibu na kasri la Buckingham hadi hoteli ya Modest iliopo karibu na eneo la Bayswater.



Gazeti hilo linasema kwamba mwezi Mei 1964, serikali ya Uingereza ilimpa Sultan huyo paundi elfu moja.


Fedha hizo zilimsaidia kuishi katika nyumba moja iliokuwa katika barabara tulivu, katika eneo la SouthSea, Hampshire. Mwaka 2000 , aliyekuwa rais wa Zanzibar Salimin Amour alimpatia uhuru Jamshid bin Abdullah.


Amor wakati huo alisema kwamba Jamshid alikuwa huru kurudi Zanzibar lakini sio kama sultan bali kama raia.


Na kwa zaidi ya miaka 56 alioishi katika hoteli hiyo iliopo karibu na ufukwe wa bahari nchini Uingereza , Sultan huyo hakuvutia watu.



Mwandishi Ned Donovan, aliyekuwa akifuatilia hadithi hiyo ya Sultan alisema: Sikupata mkaazi hata mmoja ambaye alifahamu uwepo wake , hakuzungumza na vyombo vya habari , aliishi maisha ya kunyamaza sana .


Fahamu uhusiano wa Zanzibar na Oman


Zanzibar ipo katika bahari hindi mashariki mwa pwani ya bara Afrika. Kisiwa hicho kiliungana na Tanganyika bara lakini kina rais wake na bunge ambalo linfahamika kama baraza la wawakilishi.


Baada ya kuwa kituo cha utumwa , kilivutia wakaazi wengi waliokuwa Waafrika, Waarabu, Wazungu na Wahindi.


Asili ya watu visiwani Zanzibar ni mchanganyiko wa Waafrika walio wengi, Waarabu wa Omani na Yemen mbali na Wahindi . Asilimia 98 ya wakaazi wa kisiwa hicho ni Waislamu.


Zanzibar hujulikana kama kisiwa cha karafuu kutokana na wingi wa zao la karafuu . Wakati Waarabu wa Omani walipokiteka kisiwa cha Mombasa kutoka kwa Wareno 1698, Zanzibar na Pemba zilikua chini ya watawala wa Kiarabu kutoka Omani, na baada ya zaidi ya karne moja waliondoka na kukiwacha kisiwa hicho chini ya utawala wa wakaazi.


Sultan wa kwanza kuishi Zanzibar alikuwa Saeed bin Sultan baada ya kukitembelea kisiwa hicho mara kadhaa baada ya mwaka wa 1830, wakati huo akipanua ushawishi wake katika pwani ya Afrika ya mashariki.


Baada ya kifo chake 1856 , utawala wa Sultan uligawanywa kati ya wanawe wawili ., mmoja akiwa Oman na mwengine akisalia Zanzibar, na kisiwa hicho kilikuwa chini ya utawala wa Uingereza baada ya kifo cha sultan Bargash bin Said.


Kwa sasa kisiwa hicho kipo chini ya uongozi wa rais Ali Muhammad Shein ambaye anamaliza kipindi chake madarakani mwezi Oktoba.






Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato