Afungwa minyororo chumbani baada ya kupatwa na tatizo la akili
Mkazi wa Old Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga, Shadrack Johanes (26) amefungiwa chumbani kwa miezi miwili akiwa amefungwa minyororo miguu na mikono.
Shangazi wa kijana huyo, Devota Emmanuel, alieleza kuwa baada ya kuanza kupatwa na tatizo hilo la akili, mpwa wake alianza kupiga watu, kuvunja vioo vya magari na nyumba za watu.
Kijana huyo alikutwa kwenye chumba hicho akiwa uchi, hivyo ndugu walilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kuwa amepata tatizo la akili.
Devotha alisema waliamua kumfungia ndani ili asiendelee kuwatia hasara kwasababu ya kutumia fedha nyingi kuwalipa watu waliokuwa wanaharibiwa nyumba na magari yao na kijana huyo.
Alidai kuwa walimpeleka Hospitali ya Rufani ya Bugando jijini Mwanza kupatiwa matibabu, lakini madaktari hawakubaini ugonjwa unaomsumbua, hivyo kuwapa rufani kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
"Kutokana na hali ngumu ya kimaisha na ukosefu wa fedha, tukaamua kurudi naye hapa nyumbani na kumfungia ndani ili asifanye fujo tena mitaani," Devotha alisema.
“Kijana huyu ni mtoto wa kaka yangu, baba yake yuko Bukoba na ameshakata tamaa, msaada mkubwa nimebaki ni mimi na kaka yake, na sisi hatuna uwezo wa kifedha kumpeleka huko Muhimbili, ndiyo tukaamua kumfungia ndani takribani miezi miwili sasa.
“Tumemfunga minyororo hii ili asitoroke na tukimvalisha nguo ana zichana, ndiyo maana tukaamua kumwacha aishi hivyo akiwa uchi."
"Tumeweka ndoo ya kujisaidia lakini huwa anajisaidia chini na chakula chake huwa ana kula humo humo (chumbani), na mpaka sasa hatujui tufanye nini."
Kaka wa kijana huyo, Golden Johanes, alisema imekuwa vigumu kwao kumsaidia mdogo wake kutokana na madaktari kushindwa kubaini tatizo linalomsumbua. Alisema wanaamini huenda mdogo wake huo "amechezewa kishirikina" na kwamba familia yao haina uwezo wa kifedha kumpeleka kwenye matibabu ya kibingwa Muhimbili ndiyo maana ikaamua kumfunga minyonyoro chumbani.
Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga, Panuela Samwel, alilaani kitendo hicho, akieleza kuwa ni ukatili. Aliitaka familia hiyo kumsafisha kijana huyo na kuhakikisha inamvalisha nguo, kumlaza kwenye godoro badala ya sakafuni, kumpatia chakula kwa wakati na kumhifadhi sehemu safi. Ofisa huyo wa serikali pia aliitaka familia hiyo kuhakikisha ndani ya wiki mbili kuanzia juzi, iwe imeshajipanga kifedha kumpeleka kijana huyo kwenye hospitali zinazotoa matibabu ya ugonjwa wa akili.
Comments
Post a Comment