WHO: Uongozi imara chanzo cha Afrika kupata maambukizi madogo ya corona



Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema kuwa uongozi imara wa nchi ni moja kati ya sababu za Afrika kupata kiwango kidogo cha maambukizi ya virusi vipya vya corona (covid-19), tofauti na ilivyotarajiwa.

Afrika ina 1.5% ya visa vyote vya corona vilivyoripotiwa duniai kote, na ina 0.1% ya vifo vya corona duniani kote, kwa mujibu wa WHO.

Mkurugenzi wa WHO Ukanda wa Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti alitoa kauli hiyo alipozungumza na vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, kuhusu hali ya maambukizi barani Afrika.

“Kwa kuwa na uongozi imara wa nchi zake na kutekeleza maelekezo ya wataalam wa afya kujikinga na virusi vya corona, visa vya corona barani Afrika vimebaki katika kiwango cha chini zaidi ya maeneo mengine duniani,” alisema Dkt. Moeti kwenye mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari ulioandaliwa na WHO na Jukwaa la Uchumi la Dunia (World Economic Forum).

Dkt. Moeti amesema kuwa WHO imewapa mafunzo wataalam 10,000 wa afya Afrika kwa ajili ya kusaidia kukinga na kudhibiti usambaaji wa covid-19, na kutoa huduma za matibabu.

Hata hivyo, alisema kuwa hali hiyo haiwezi kuwa kigezo cha kuacha kuchukua tahadhari zaidi dhidi ya covid-19, na kwamba anazisihi nchi za Afrika kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya virusi hivyo.

Jumla ya watu milioni 6.05 wameripotiwa kupata virusi vya corona barani Afrika, watu milioni 2.56 kati yao wamepona na 369 wamepoteza maisha.

Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zimeripoti idadi ndogo ya visa vya corona Afrika, ikiwa imeripoti visa 509 na vifo 21. Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), alikataa kutumia njia ya kuwafungia wananchi ndani (lockdown), badala yake akaongeza elimu na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi na kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya. Pia, aliwasihi kutumia tiba asili katika kupambana na virusi hivyo.

Shughuli zote nchini Tanzania zinaendelea ikiwa ni pamoja na usafiri wa anga. Sekta ya utalii imefunguliwa na watalii kutoka nje ya nchi wanaingia bila masharti ya kuwekwa karantini kwa siku 14.




Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato