Wanaodaiwa kuwa wapenzi wakutwa wamejinyonga
WATU wawili; Jackson Hamis (24) na Lenista Mligo (24) wakazi wa Making’inda Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambao wanadaiwa kuwa ni wapenzi, wamekutwa wamefariki dunia kwa kujinyonga katika maeneo mawili tofauti, huku mazingira ya vifo vyao yakiwa ni ya kutatanisha.
Akizungumza juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maingwa, alisema tukio hilo lilitokea Mei 29, mwaka huu saa 1.30 asubuhi katika maeneo tofauti yaliyopo Kata ya Msamala, Mtaa wa Making’inda, Manispaa ya Songea.
Kamanda Maigwa alilitaja tukio la kwanza kuwa ni la Lenista ambaye alikutwa kwenye mti akiwa amejinyonga kwa mtandio, huku miguu ikiwa imegusa chini ya ardhi jambo ambalo alisema linatiliwa shaka kama amejinyonga mwenyewe au kauawa na kuwekwa kichakani hapo.
Alisema tukio la pili ni la Hamis aliyekutwa chumbani alimokuwa akiishi akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka ambalo alifunga juu ya kenji ya nyumba hiyo.
Kamanda Maigwa alisema kabla ya tukio hilo, wapenzi hao walionekana wakinywa pombe za kienyeji na inadaiwa waliondoka eneo hilo wakiwa na ugomvi baada ya mwanaume kumuhisi mwenzi wake kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mtu mwingine.
Alifafanua kuwa Lenista alikuwa na mtoto mdogo ambaye anakadiriwa kuwa na miaka miwili na alikutwa akiwa hai huku akiwa amelala kando ya mwili wake.
Comments
Post a Comment