RC Malima: Hospitali Rufani Mara mbioni, huduma kutikisa
NI simulizi inayochukua miaka 40 na kadhaa, leo hii kunatekelezwa wazo la Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, kujengwa Hospitali ya Rufani Mkoa Mara, katika kitongoji cha Kwangwa ndani ya Manispaa ya Musoma.
Mkuu wa Mkoa, Adam Malima, anasema ni uamuzi uliorejeshwa tena katika utekekezaji kupitia mikakati ya kufufua mipango mbalimbali ya Mwalimu Nyerere.
Ni mradi unaoatarajiwa kunufaisha wakazi kutoka wilaya za Butiama, Rorya, Tarime, Musoma Mjini, Musoma Vijijini na Serengeti, pia majirani na wageni wao.
Pia, Manispaa mjini Musoma, ambako kwenye mradi unaotekelezwa kwa jina la Mwalimu Nyerere Memorial Hospital, ulioko katika mwambao wa Ziwa Victoria.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, anasema hospitali hiyo inajengwa katika eneo lililopo mbali wa kilomita mbili, Kusini mwa mjini Musoma, kwenye mwinuko ukipambwa na madhari ya Ziwa Victoria.
Anasema, ujenzi wa hospitali hiyo ulianza mwishoni mwa mwaka jana, baada ya Rais Dk, John Magufuli, kuidhinisha zaidi ya Sh. bilioni 15.
Malima anasema, ni ujenzi unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na tangu kazi hiyo ianze, kuna hatua kubwa iliyopigwa kupitia mradi.
Mkuu wa Mkoa anasema mipango waliojiwekea ni hadi kufikia Julai ijayo, ujenzi uwe umekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa mkoani, hata wageni wa nchi jirani.
"Hospitali hii haitakuwa ya Rufani ya Mkoa, bali itakuwa ya kibingwa na kibobezi kwa baadhi ya huduma na itatoa huduma kwa wananchi wote wa Kanda ya Ziwa," anajigamba Malima, huku akiwataja wa mikoa na nchi jirani nao ni wanufaika.
"Kukamilika hospitali hii itakuwa mkombozi kwa wananchi wa mkoa wa Mara ambao watakuwa wakipata huduma za hospitali ya rufani katika mkoa wao tofauti na sasa wanalazimika kwenda Bugando, Mwanza," anaongeza.
SAFARI YA UJENZI
Malima anasema, ujenzi wake ulianza na mkakati wa pamoja kimkoa katika vikao vya pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Anawataja washiriki wengine aliokuwa nao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na wawakilishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambao ndiyo makandarasi.
Pia, anamtaja mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Ardhi ambaye ndiye Mshauri Mwelekezi katika mradi huo na maofisa waandamizi wa serikali.
"Baada ya kikao hicho kazi ya ujenzi inafanyika usiku na mchana kuhakikisha hospitali inakamilika haraka, ili kuhakikisha huduma zinaanza kutolewa kwa muda uliopangwa," anasema.
Mkuu huyo wa Mkoa anasema, jengo la hospitali hiyo limepitia kwa makandarasi wawili, kabla ya NHC kukabidhiwa kazi na limefanyiwa maboresho, ili kuwa na huduma zote za kiwango cha hospitali za rufani.
Mkuu wa Mkoa anasema, katika kufanikisha mradi kumekuwapo ziara za kila mara zinazofanywa na viongozi wa kiserikali kukagua na kusaidia kutatua changamoto zinazoukabili mradi, ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Malima anasema, ni hospitali ya ghorofa tano, ikichukua eneo kubwa la mita za mraba 24,482 na majengo mengine ya pembeni yenye mita za mraba 1,039, yaliyogawanyika katika sehemu kuu tatu.
MPANGO AFYA
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo ya Afya (MMAM) ulioanza kutumika miaka 12 iliyopita, kila kijiji au mtaa kwa mijini, kunapaswa kuwepo zahanati na kata kuwa na kituo cha afya.
Vivyo hivyo inaelekeza kwamba, katika ngazi ya wilaya kunatakiwa kuwapo hospitali na mikoa, hospitali zake sasa zitakuwa za rufani na juu yake katika ngazi ya kanda, kama ilivyo Bugando na Mbeya na Muhimbili imekuwa ya taifa.
Hata hivyo, katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, hospitali za manispaa; Temeke, Amana iliyopo wilayani Ilala na Mwanayamala (Kinondoni), zimekuwa za rufani katika hadhi inayofanana na mikoa.
Pia, bado malengo hayajatekelezwa kukidhi wastani wa mahitaji ya mpango MMAM kitaifa, kama ilivyokuwa katika mkoa Mara.
Katika baadhi ya mikoa, serikali kihistoria imekuwa ikiingia katika ubia na hospitali binafsi, hususan na taasisi za kidini na kuwa wawakilishi wa serikali, hivi sasa katika ngazi mbalimbali za MMAM, mpango wenye zaidi ya miaka 10 sasa.
SERA INAVYOELEKEZA
Sera ya Afya nchini, inafafanua kwamba hospitali nchini zinapaswa kupatiwa vifaa vya hali ya juu, ziweze kutibu magonjwa yote ambayo hivi sasa yanapelekwa watu nchi za nje kwa tiba ya ziada.
Pia, inahimiza umefika wakati hospitali hizo kuwa na ‘ubingwa maalum’na katika hilo hospitali ziteue’ubingwa’ kuendana na vifaa vya kuhudumia ubingwa huo, kupunguza safari za kupeleka wagonjwa nje.
Lingine, ni hospitali hizo zinahitaji wodi nyingi, kutosheleza mahitaji ya ubingwa maalum, ikiwa ni pamoja na huduma za dharura na uangalizi maalum (ICU).
Pia, inaelekeza hospitali ya rufani kuwa na vitanda kati ya 400 na 600 na wakati wa andiko la sera hiyo, hospitali za rufani nchini zilikuwa na vitanda kati ya 420 na 1,425.
“Ngazi hii iwe na mchanganyiko wa wataalamu wenye taaluma za hali ya juu kabisa, ili kuweza kutekeleza barabara majukumu mengi ya kutoa huduma za tiba na kinga, kufundisha na kufanya utafiti,” inafafanua sera hiyo.
Pia, inagusia wigo wa vinavyotakiwa kupatikana katika hospitali za rufani ni: Tiba za kawaida, lakini kwa weledi wa juu; mafunzo ya wataalamu wapya na wa kujiendeleza; kufanyika utatifi; utoaji ushauri wa kitaalamu kuhusu afa nchini; kutembelea hospitali nyingine katika kanda (out-reach) ili kutoa ushauri wa karibu na mafunzo kwa wataalamu wa huko.
“Hospitali za rufani zitahitaji vyombo vingi vya usafiri kuliko hospitali za mikoa, ili kuwawezesha wataalamu wa hospitali hizo kutekeleza majukumu yao,” inaeleza sera hiyo.
Comments
Post a Comment