Kanuni Ligi Kuu Z'bar kuboreshwa
SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF), limeanza mchakato wa kufanya maboresho ya Kanuni za Mashindano kwa ajili ya msimu ujao wa mwaka 2020/21, imeelezwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa ZFF, Ali Mohammed Ameir, alisema katika mchakato huo wameanza na zoezi la kupokea maoni kutoka kwa wadau wa soka wa visiwani hapa ili kupatikana kwa kanuni mpya za mashindano.
Ameir alisema kila mtu anayo fursa ya kutoa maoni juu ya kanuni ya kuendesha mashindano kwa msimu wa mwaka 2020/21 na ZFF inaahidi itayafanyia kazi maoni hayo ili kupata kanuni bora katika uendeshaji wa ligi zake.
"Tunaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau wa soka wa hapa Zanzibar ili kupata kanuni ya kuendesha mashindano, miongoni mwa mambo katika kanuni hiyo ni muundo wa ligi utakavyokuwa, ikiwamo Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi za Vijana, na zile za wanachama wetu ikiwamo Ligi za mikoa na wilaya," Ameir alisema.
Aliongeza kutokana na changamoto ya kukutana uso kwa uso na wadau kwa sababu ya kuwapo kwa ugonjwa wa corona, ZFF pia inapokea maoni kupitia njia ya mitandao ya kijamii pamoja na barua pepe ya shirikisho hilo.
Kiongozi huyo amewataka wadau mbalimbali wa michezo kutoa maoni yao bila kusika kwa sababu wanaamini ndiyo yatasaidia kuboresha, kuendesha na kusimamia ligi katika ubora unaotakiwa.
Comments
Post a Comment