Vijana waaswa kuunga mkono jitida za Serikali katika mapambano hidi ya corona
Na Thabit Madai,Zanzibar.
VIJANA Nchini wametakiwa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kukabiliana na maradhi ya mripuko ya Corona.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir wakati alipokuwa akigawa vifaa mbali mbali vya kujikinga na maradhi Corona huko Baraza la Vijana Mwanakwerekwe.
Aliwataka vijana kuwa makini katika kupambana na maradhi hayo kwani hivi sasa yamekwisha sambaa duniani kote
‘Nyinyi ndio taifa la kesho hivyo wekeni tahadhari kujikinga na maambukizo kwa kufuata taratibu na miongozo ya serikali inayotolewa na Wizara husika na kuacha kufanya mzaha tatizo ni kubwa,” alisema Mwenyekiti huyo.
Aliwataka vijana hao kuacha kusikiliza taarifa zisizothibitiishwa na kutolewa na serikali zote mbili kwani kufanya hivyo kutawajengea hofu.
Aliwafahamisha vijana hao kutumia fursa ya kuzungumza ugonjwa wa Corona katika maeneo yao na kuielimisha jamii jinsi ya kujikinga kwa lengo la kuepuka kusambaa zaidi .
Aliwaelekeza vijana kutumia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ili maradhi hayo yaishe na kuwafanya watu waendelee na shughuli zao za kiuchumi.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar Kombo Mohamed Khamis amesema mashirikiano ya Baraza la Vijana na Jumuiya hiyo itasaidia kushajihisha vijana kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na janga la Corona .
Dunia hivi sasa inakabiliwa na janga kubwa la maambukizi ya maradhi ya corona yanayotokana na virusi vya aina ya COVID -19 ambayo yalianzia nchini China katika Mji wa Wuhan September 2019 mwaka jana na kusambaa nchi mbali mbali ulimwenguni.
Comments
Post a Comment