Mwanaume ajiandalia jeneza kisa mateso ya familia
Na Paschal Malulu, Kahama
Mkazi wa Ushirombo kitongoji cha Butambala Kata ya Igulwa wilayani Bukombe mkoa wa Geita Sylvester Mihayo (45) anaishi na jeneza ndani ya nyumba ambalo ameliandaa kwaajili ya mazishi yake pale atakapofariki kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kuchoshwa na kunyanyaswa na familia yake.
Aidha mwanaume huyo akizungumza na waandishi wa habari alieleza kuwa kwa takribani miaka 3 sasa, anaishi bila furaha kutokana na unyanyasaji huo ikiwa ni pamoja na kipigo kutoka kwa mke na watoto wa kuwazaa mwenyewe hali iliyompelekea kuitelekeza nyumba na kuishi kwenye karakana ya ufundi anakochomelea kwa kutumia mitungi ya gesi.
Alisema kuwa chanzo cha mateso yake ni baada ya kuugua kwa muda mrefu tangu mwaka 2018 ambapo familia ilimtenga na kumzuia kuingia kwenye nyumba yake kwa madai kuwa siyo yak wake badala yake ni nyumba ya urithi kwa watoto wake.
“Ndugu zangu waandishi wa Habari mimi kujichongea jeneza siyo kwamba nitajidhuru, bali nimejitabilia kufa kutokana na manyanyaso na ukatili naofanyiwa na familia yangu na litatumika kama mauti yatanikuta, ninamiaka mitatu nateseka na ugonjwa na sina msaada wa familia katika matibabu walichokifanya wamenikimbia name nikarudi kuishi kwenye ofisi yangu ya karakana ya ufundi huu ugonjwa haueleweki,” alisema Mihayo kwa huzuni na kuongeza.
“Kwa sasa familia yangu, wamejenga nyumba nyingine eneo la Maghorofani Ushirombo ili waendeshe uganga wao kwa uhuru kwa kipindi chote hicho wakati huo nikiwa nasaka matibabu katika hospitali zote ambazo nazo zimekosa ugonjwa wakiwamo waganga wa jadi ndipo kipindi cha 2018 nikachongesha jeneza kwa maandalizi ikitokea nimefariki litatumika hilo,” alisema Mihayo huku akibubujikwa na machozi.
Hata hivyo, mke wake Vumilia John hakupatikana kuzungumzia hali hiyo baada ya kuondoka nyumbani kwake, na hata alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya kiganjani alikataa kwa madai ya kumuuguza mgonjwa mwingine wilayani Kahama.
Mama mzazi wa mwanaume huyo Veronika Kasase (86)mkazi wa kijiji cha Mwalo Kata ya Businda Halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani hapa akizungumza na waandishi wa Habari nyumbani kwake huku akimwaga machozi wakati akisimulia mkasa wa mwanaye alisema mwanaye amegeuzwa msukule kwa imani za ushirikina.
Alisimulia kuwa mwanaye anamiaka mitatu nateseka na ugonjwa usiofahamika na kwamba ametumia fedha nyingi na hospitali nyingi hapa nchini hadi kwa waganga wa jadi lakini hakuna nafuu badala yake aliambulia kutolewa maji mengi tumboni yenye ujazo wa lita nane pamoja na kunyofolewa nyama ubavuni ambayo ilipimwa na kukosekana kansa.
Hata hivyo mama alieleza kuwa alishitushwa na kitendo cha mwanaye kumweleza kuwa amechonga jeneza kwaajili ya kuhifadhi mwili wake pindi mauti yatakapomkuta kutokana na kushindikana matibabu kwa kipindi chote hali ambayo alimtaka alilete nyumbani kuliko kukaa nalo huko.
“Mimi nilijaribu kuwaita ili nijue chanzo cha wanangu kusambaratika kiaina ukilinganisha ni watu wazima sasa na wanafamilia kubwa ya watoto wanane kisha nipate nafasi ya kuwashauri wake pamoja na kuuguzana lakini mkamwana wangu alikataa kabisa jambo ambalo tumemwachia mungu,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita Said Nkumba akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema hajapata taarifa za Mihayo na kuahidi kumtafuta ili kupata maelezo ya kina kwaajili ya ufumbuzi wa suala hilo.
“Suala la kujiandalia jeneza siyo jambo la kushangaza sana ama kuleta taharuki kwa jamii lakini niwapongeze sana kwa kusaidia wananchi kama mkuu wa wilaya hii nimeletwa na rais kushughulikia na kutatua kero za wananchi na kama mwakilishi wake hili suala nitalishughulikia kwa kiwango kikubwa na nitawaita wote mke na mume tukae na wasaidizi wangu kwa maana ya ustawi wa jamii na ngazi zingine tulipatie ufumbuzi,” alisema Said Nkumba mkuu wa wilaya ya Geita.
Comments
Post a Comment