Yanga, Alliance hapatoshi leo
HATUKUBAHATISHA! Hayo ni maneno ya Yanga kuelekea mechi yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Alliance FC kutoka Mwanza inayotarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Yanga itashuka dimbani katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare nne mfululizo katika mechi za ligi huku Alliance ikiwa na kumbukumbu ya kumchapa Mwadui FC mabao 4-1.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema timu yake iko tayari kwa mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani na wachezaji hawana hofu ya aina yoyote.
Mkwasa alisema wamejipanga kuendeleza kasi ya ushindi na wanaamini wakifanya vizuri katika mechi zao zinazofuata, wana nafasi ya kuutwaa ubingwa wa ligi ambao sasa unashikiliwa na watani zao Simba.
"Maandalizi yetu ni mazuri, timu haina hofu yoyote kuelekea mechi ya kesho (leo), kama baadhi ya mashabiki wenye lengo la kuwavuruga wachezaji wao kisaikolojia wanavyodai, na kuelekea pia katika mchezo wa dhidi ya Simba tutakaocheza Machi 8, mwaka huu," alisema Mkwasa.
Kocha huyo alisema wanaifahamu Alliance FC na kuitambua ni moja ya timu zinazoundwa na wachezaji wenye vipaji na wanaocheza kwa kasi, hivyo wamejipanga kukabiliana na changamoto hiyo.
Aliongeza ushindi walioupata katika mechi dhidi ya Gwambina FC katika mashindano ya Kombe la FA, imewaongezea morali wachezaji wake na kila mmoja amejiandaa kuisaidia timu kuondoka na pointi tatu.
"Tutaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa, tunaiheshimu Allinace na kamwe hatuwezi kuibeza, mechi zote ni ngumu na hii inatokana na namna timu zilivyojipanga kwa kuhofia kushuka daraja," Mkwasa alisema.
Alieleza anafahamu mashabiki wa Yanga wanahitaji kuona timu yao inapata ushindi na kuona burudani ambayo itawarejesha kwenye mbio za kuwania ubingwa baada ya kukata tamaa iliyotokana na matokeo ya sare nne walizopata katika mechi zilizopita.
Nahodha wa Yanga, Juma Abdul, aliliambia gazeti hili wachezaji wote wako tayari na kamili kupambana na hatimaye kupata pointi tatu.
"Hakuna mechi nyepesi, lakini tumeshaona upungufu wetu, tutataka kumaliza unyonge, tumejipanga kurejesha heshima, tunaamini tutafanikiwa kupata tunachokitafuta," alisema beki huyo.
Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya Mwadui FC dhidi ya Coastal Union, Kagera Sugar vs Tanzania Prisons, Ruvu Shooting vs Mbao FC, Lipuli vs Namungo, Biashara United vs Mbeya City, Mtibwa Sugar vs Ndanda na JKT Tanzania wataialika Azam FC.
Comments
Post a Comment