Waziri Jafo afungua kongamano la Mama Lishe Festival Kisalawe


WAZIRI wa Ofisi ya Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo, amesema kukamilika kwa mradi wa maji  ulioigharimu Serikali kiasi cha zaidi ya Sh Bilioni 10, kutazidi  kukuza maendeleo ya wilaya hiyo ambayo kwa kipindi cha hivi karibuni imeshuhudiwa ikipiga hatua kubwa kupitia sekta za elimu pamoja na afya.

Akizungumza wakati akifungua kongamano la ‘Mama lishe’ lililowakutanaisha mama lishe mbalimbali wilayani humo, Waziri Jafo  pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo kutokana na  juhudi  mbalimbali anazozichukua kuchagiza kasi ya maendeleo ya wilaya hiyo akisisitiza kuwa ana jisikia fahari kumpata Mkuu huyo wa wilaya ambaye ni ‘mchapakazi’

Alisema  kuanza kupatikana kwa huduma ya maji safi na salama ambayo hapo zamani ilikuwa kero kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo, ni jambo walilolipokea kwa furaha wananchi wa Kisarawe na kuongeza kuwa pamoja na hiyo,  huduma zingine muhimu zinazopatikana wilayani humo kunazidi kupeleka mbele maendeleo ya wilaya hiyo ya Kisarawe.

“Ni wazi kuwa wilaya ya Kisarawe inazidi kukua, ukitazama sekta ya afya tupo safi, elimu nayo kupitia kwa Mkuu wa Wilaya wetu inazidi kupiga hatua na hivi sasa kuanza kupatikana kwa huduma ya maji kunazidi kutupeleka mbele kimaendeleo” alisema Waziri Jafo na kuwataka wananchi hao kutembea vifua mbele.

Aidha katika kongamano hilo lililoudhuriwa na viongozi mbalimbali  akiwemo Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati Subira Mgalu, Waziri Jafo pia aliipongeza wilaya hiyo kwa kuitikia wito wa Waziri Mkuu  kwa kuhamasisha wananchi wake   kuhusu  masuala ya lishe hatua ambayo pamoja na mambo mengine italiwezesha Taifa kupiga hatua dhidi ya changamoto ya tatizo la utapiamlo.

Alisema  siku za hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa maelekezo kwa Mikoa yote nchini kuhakikisha wanachukua hatua madhubuti katika kuhamasisha suala la lishe kwa wananchi wao ili kupunguza tatizo la utapiamlo linaloonekana kuwakabili idadi kubwa ya watoto hapa nchini na hivyo kutishia usalama wa maisha yao.

“Niipongeze Wilaya ya Kisarawe kwa kuitikia wito huo wa kuwahamasisha wananchi kuhusu suala la lishe ambapo katika kongamano hilo suala hilo mmelichukua kama moja ya jambo muhimu, kikubwa tukifanikiwa kufanya hivyo katika maeneo mengine tutaweza kukabiliana na changamoto ya utapiamlo” alisema Jafo.

Aidha amewataka wanawake wa wilaya hiyo kujiunga katika vikundi mbalimbali vya  ujasiriamali suala litakalowafanya waweze kupewa mikopo itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi sambamba na kujiletea maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.

Alisema kuna fursa nyingi zinazoweza kuwafikia wananchi endapo watajiunga katika vikundi ikiwemo kupewa mikopo itakayowawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo ikiwemo kuziongoza familia zao katika misingi imara ya kimaisha.

Awali Mkuu wa wilaya hiyo Jokate Mwegelo alisema kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo ‘Mama lishe ni msingi wa lishe Bora na uchumi endelevu” limeandaliwa maalumu wakati huu wa kuelekea siku ya wanawake Duniani  likilenga kuwachochea wanawake ili waweze kuyafikia maendeleo yenye usawa wa kijinsia.

Alisema sababu nyingine ya kuandaliwa kwa kongamano hilo, ni kuwaongezea uwezo, ujuzi na elimu mama lishe kwenye usafi wa vyakula, thamani yao pamoja na kuwatengenezea mtandao wa kibiashara na wadau mbalimbali walioko ndani na nje ya wilaya hiyo.

“Kongamano hili pia limekusudia kuwajenga mama lishe katika masuala ya mapishi kwa kuzingatia mlo kamili ili kuondoa udumavu na utapimlo, lakini pia kuwashindanisha wanawake wanaofanya shughuli za mama lishe ili kuweza kuboresha mapishi na hivyo kujiongezea kipato” alisema Jokate

Alisema anaamini baada ya kongamano hilo, wanawake hao wataweza kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao na  pia kujiweka katika mazingira mazuri ya ushindani katika mapishi mahali popote pale watakapata nafasi za kushiriki katika suala zima la mapishi.

Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato