Simba, Yanga kuonyeshana ubabe machi 8

MECHI ya marudiano ya watani wa jadi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20, Yanga dhidi ya Simba imepangwa kufanyika Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa na Bodi ya Ligi kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana mwenyeji wa mchezo huo ambao wa raundi ya 28 ni Yanga inayofundishwa na Kocha Mkuu Mbelgiji Luc Eymael.

Katika mechi hiyo, timu hizo zitashuka dimbani zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2, ambayo walipata katika mchezo wa mzunguko wa kwanza iliyochezwa Januari 4, mwaka huu jijini.

Matokeo hayo bado yamekuwa yakiwaumiza mashabiki wa Simba baada ya kuamini timu yao ingeondoka na pointi tatu na yakionekana kufurahiwa na Yanga ambayo ilidhani 'jahazi' lao limezama baada ya kuwa nyuma kwa magoli 2-0.

Magoli ya Simba inayonolewa na Sven Vandenbroeck, raia wa Ubelgiji katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jonesia Rukyaa kutoka Bukoba yalifungwa na Meddie Kagera na Deo Kanda huku ya Yanga yakipachikwa kimiani na Mapinduzi Balama na Mohammed Issa 'Banka'.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Simba itashuka dimbani kesho kuwakaribisha Coastal Union kutoka jijini Tanga na Februari 4, mwaka huu itawavaa Polisi Tanzania, mechi zote zikichezwa jijini wakati Mtibwa Sugar itawafuata Yanga Jumapili na Februari 5, mwaka huu itacheza dhidi ya Lipuli FC ya mkoani Iringa.

Yanga ambayo ina mechi pungufu, itashuka tena uwanjani Februari 8, mwaka huu ikiwa mgeni wa Ruvu Shooting na siku tatu baadaye itawakaribisha Mbeya City wakati Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kuwavaa wenyeji Mtibwa Sugar na baada ya hapo itaelekea Iringa kucheza dhidi ya Lipuli FC hapo Februari 15, mwaka huu.

Ratiba hiyo inaonyesha raundi ya tano ya mechi za mashindano ya Kombe la FA zitachezwa kati ya Februari 25 na 26 mwaka huu huku msimu ukipangwa kumalizika katikati ya Mei.

Hata hivyo, mapema jana Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Stephen Mguto, alisema ofisi yake 'ilijisahau' kuwapangia Yanga mechi katikati ya wiki hii kwa ajili ya kumaliza 'viporo' walivyonavyo.

"Vijana wangu walijisahau kuwapangia Yanga mechi katikati ya wiki hii baada ya kumaliza mchezo wao wa Kombe la FA, walipaswa kucheza katikati ya wiki kama zilivyocheza timu nyingine," Mguto alisema.

Simba itafunga pazia la msimu huu kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi dhidi ya wenyeji Polisi Tanzania wakati Lipuli FC itawakaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa.

Mabingwa watetezi Simba ambayo imecheza mechi 17, ndio vinara wakiwa na pointi 44 wakati Ndanda FC ya Mtwara iliyoshuka dimbani mara 17 na ina pointi tisa, inaburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20.

Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato