TANROADS waombwa kuboresha barabara Simiyu
Na James Timber-Simiyu
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amezipongeza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Simiyu kwa kazi nzuri zinazofanya na kuzisisitiza kutenga bajeti ya kuboresha ujenzi wa Barabara zote zinazounganisha Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine ili zipitike wakati wote.
Kiswaga ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Simiyu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Desemba 30, 2019 mjini Bariadi ambapo amebainisha kuwa barabara zikiboreshwa zitarahisisha usafiri kwa wananchi na usafirishaji wa malighafi mbalimbali za viwanda na bidhaa zitakazozalishwa na viwanda, vinavyotarajiwa kujengwa Mwaka 2020.
“Kazi inayofanywa na TANROADS na TARURA ni kazi ambayo inatia moyo na itakuwa na mchango mkubwa kwa viwanda vya nguo, glasi na vifaa tiba vitakavyoanzishwa mwakani; kwa maana ya material(malighafi) itakayoingia na bidhaa zitakazotengenezwa zitasafirishwa kwa urahisi,” alisema Kiswaga.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. John Mkumbo amesema katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2019/20 kazi za matengenezo ya barabara ambazo zipo kwenye utekelezaji ni kilometa 108.12 na madaraja 14.3 sawa na 54.3% huku iliyokamilika kwa barabara kuu ni kilometa 246.52 na madaraja 19.71 sawa na 40.8%.
Kwa upande wake Mratibu wa TARURA mkoa wa Simiyu Mhandisi Dkt. Philemon Msomba amesema kuwa wametekeleza jumla ya miradi 30 ambayo tayari imekamilika yenye thamani ya shilingi 3,694,627,194 bila VAT .
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Meatu, Dkt Joseph Chilongani amesema ni vyema wakala wa barabara nchini (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuboresha madaraja yaliyopo wilaya ya Meatu kwa kujenga madaraja ya juu badala ya yale yaliyopo sasa ambayo ni ya chini ili barabara hizo zipitike wakati wote.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Enock Yakobo aliwataka wakala hao kuweka taa kwenye maeneo ya katika ya miji ili wananchi waweze kufanya biashara zao nyakati zote ( saa 24).
Mbunge wa Busega, Mhe. Dkt. Raphael Chegeni ameshauri kuwa ni vema Serikali ikafanya marekebisho katika mgao wa fedha za bajeti ya barabara kati ya wakala Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kutoka kwenye uwiano wa sasa, ambapo TANROADS inapata asilimia 70 na TARURA asilimia 30, iwe asilimia 40 kwa TARURA na asilimia 60 kwa TANROADS ili kuongeza ufanisi kwa TARURA.
Comments
Post a Comment