Hakuna kuidhinisha matumizi kabla ya kutenga mikopo ya vijana, wanawake na walemavu - Dkt. Mabula
Na James Timber-Mwanza
Baraza la Madiwani la halmashauri ya manispaa ya Ilemela limekubaliana kwa pamoja kutopitisha matumizi yeyote ya fedha za mapato ya ndani kabla ya kutenga asilimia kumi ya fedha hizo kwaajili ya mikopo ya wanawake 4%, vijana 4% na watu wenye ulemavu 2%.
Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wananchi wa kata za Ilemela, Kawekamo na Pasiansi ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuvitembelea vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinavyopatikana katika jimbo lake kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili katika sekta ya mikopo na kuzipatia ufumbuzi ambapo amesema kuwa Serikali imezielekeza halmashauri zote nchini kufungua akaunti maalumu kwaajili ya kuhifadhi fedha zitakazotumika kukopesha makundi hayo
"Tumekubaliana katika baraza la madiwani hakuna kuidhinisha matumizi ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani kabla ya kutenga fedha za mikopo katika akaunti yake maalumu," alisema.
Aidha Mhe Dkt Mabula ameishukuru Serikali kwa kufuta riba ya mikopo hiyo sanjari na kupunguza gharama za usajili wa vikundi kufikia elfu thelathini huku akiwaomba vijana waliopata mafunzo ya kitalu nyumba kutoka wizara ya ofisi ya waziri mkuu vijana kazi na ajira na wale waliopata mafunzo ya utaalamu wa ngozi kujitokeza na kufundisha wengine ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela, Shukrani Kyando amesema kuwa manispaa yake imekwisha tekeleza agizo la Serikali la kufungua akaunti maalumu kwaajili ya kuhifadhia fedha za mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu sanjari na kuwaasa vijana kutumia fursa hiyo ya mikopo kuanzisha miradi mbalimbali itakayowasaidia kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira badala ya kuachia kundi la wanawake peke yao wanaotumia vizuri fursa hiyo.
Nae afisa maendeleo ya jamii wa manispaa hiyo ambae pia ni mratibu wa mfuko wa wanawake Bi Amina Bululu amevitaka Vikundi vilivyokuwa vimesajiliwa kabla ya kuanzishwa kwa manispaa ya Ilemela mwaka 2012 kukamilisha taratibu za usajili katika manispaa ya Ilemela vinapofanyia kazi kwa sasa tofauti na hapo awali vilipofanya usajili huo katika halmashauri ya jiji la Mwanza.
Akihitimisha katibu wa kikundi cha walemavu Bwana Richard Kashinje ameiomba Serikali kuongeza fedha wanazotengewa watu wenye ulemavu kiasi cha 2% ya mapato ya ndani baada ya makusanyo ili waweze kuwa na mtaji wa kutosha utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuacha kuonekana kama kundi tegemezi lisiloweza kufanya chochote katika jamii.
Comments
Post a Comment