Aiba Kichanga Anusurika kifo

Mama mmoja, mkazi wa Kitongoji cha Mwanzugi wilayani Igunga Mkoa wa Tabora aliyejifanya mjamzito, Shija Mihambo (32) amenusa kifo baada ya kupigwa na wananchi kwa tuhuma za wizi wa kichanga.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk Deus Rutha alisema, tukio hilo wiki iliyopita muda wa saa moja asubuhi kwenye wodi ya wajawazito.

Dk Rutha alisema, akiwa nyumbani kwake, alipigiwa simu na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Dk Merchades Magongo akimjulisha kuna wizi wa kichanga.

Alisema alikwenda hadi hospitalini hapo ambapo alikuta wananchi wengi, huku mtuhumiwa akiwa tayari amekamatwa na mganga mfawidhi kwa kushirikiana na wananchi.

Alisema mama huyo, alikamatiwa maeneo ya stendi kuu ya mabasi saa 1:48 asubuhi akiwa na kichanga hicho chenye uzito wa kilo 3.3 cha jinsi ya kike akiwa kwenye pikipiki aliyokodi kwenda Kitongoji cha Mwanzugi.

Dk Rutha alimtaja mama aliyeibiwa mtoto kuwa ni Hoka Maganga, mkazi wa Kijiji cha Bulenya Kata ya Nanga ambaye alifika hospitalini hapo Desemba 13, mwaka huu, saa 2 usiku akiwa mjamzito ambapo alilazwa na ilipofika saa 6:00 usiku kuamkia Desemva 14, alijifungua mtoto wa kike.

Alisema tayari mtoto amekabidhiwa kwa mama yake na afya yake inaendelea vizuri na mtuhumiwa alifikishwa kituo cha polisi kwa hatua zaidi akaongeza kuwa hilo ni tukio la pili ndani ya miezi mitano kutokea hospitalini hapo.

Alisema wamejipanga kuimarisha ulinzi kwa kila mtu anayeingia na kutoka hospitalini hapo.

Mmoja wa kina mama waliolazwa hospitalini na mwanae, Joyce John walisema mama huyo aliingia wodi ya wazazi saa 8:00 usiku akiwa amejivingirishia nguo tumboni ili kuonesha yeye ni mjamzito, huku akiwa na beseni ambapo wao waliamua kunyamaza.

Mama wa mtoto, alisema mama aliyemuibia mtoto alimuomba amwangalizie aende kujisaidia na aliporudi alikuta kaondoka na mwanawe ndipo akaanza kuomba msaada.

“Uaminifu umekwisha, nilimuachia mwanamke mwenzangu aniangalizie mwanangu ili niende kujisaidia, kumbe ni mwizi, namshukuru Mungu na uongozi wa hospitali ulioongozwa na mganga mfawidhi kwa kumkamata mwizi wa mwanangu,” alisema.

Mtuhumiwa huyo alikiri kuiba kichanga hicho na kusema alifanya hivyo siyo kwa nia mbaya, kwani angeenda kumtunza.

Ofisa Mtendaji Kata ya Igunga, Robert Mwagala alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema polisi walifika hospitali kuwatuliza wananchi waliojaa hasira.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Barnabas Mwakalukwa alipotafutwa ili aweze kuzungumzia swala hili alisema upelelezi ukikamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.


Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato