Serikali yaombwa kutatua tatizo la magunia Masasi
Na Hamisi Abdulrahmani, Masasi.
Serikali imeombwa kuingilia kati suala la tatizo la ukosefu wa magunia ya kuhifadhia korosho za wakulima wilayani Masasi mkoani Mtwara ambapo bado korosho nyingi za wakulima zipo majumbani mwao na zinashindwa kupelekwa katika minada kutokana na tatizo hilo.
Hayo yalisemwa jana wilayani Masasi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi kwenye kikao chao cha kawaida cha baraza la Madiwani kilichofanyika katika kijiji cha Mbuyuni makao makuu mapya ya Halmashauri hiyo.
Walisema kuwa korosho nyingi bado zipo majumbani kwa wakulima zimehifadhiwa sakafuni na kwamba zinashindwa kukusanywa na kupelekwa katika minada inayofanyika kutokana na uhaba wa magunia.
Walisema hata idadi ya korosho zilizouzwa kwenye minada na zilizopo kwa wakulima kwa kukosa magunia idadi kubwa zile ambazo zimekwama kwa kukosa magunia ya kuhifadhia.
Musa Msanga diwani kata ya Lulindi alisema wanaiomba serikali kuingilia kati suala la uhaba wa magunia kwa wakulima.
Alisema korosho bado zipo kwa wakulima na ni wazi kuwa wakulima wengi kwa sasa wanashindwa kupeleka korosho zao katika minada kwa sababu hawana magunia ya kuwekeza mazao yao.
Alisema kata ya Lulindi ina wakulima hivyo bado zao wanashindwa kuzipeleka kwenye minada kwa vile hawana magunia ya kuwekea korosho kabla ya kuzipeleka ghalani kwa ajili ya kuingia mnadani.
Naye diwani kata ya Lupaso alisema tatizo hilo la uhaba wa magunia katika chama kikuu cha wakulima Masasi-Masasi( MAMCU) zinaweza kufanya korosho nyingi za wakulima zikabaki bila ya kuuzwa na minada ikawa imefungwa.
Alisema serikali ichukuwe hatua za masukudi kuingilia kati na kutafutia ufumbuzi tatizo hili la uhaba wa magunia ambapo imekuwa kero kwa wakulima.
Naye diwani kata ya Nangoo, Mohammed Chilumba alisema kila mwaka tatizo la uhaba wa magunia limekuwa likijitokeza hivyo kufanya korosho nyingi kushindwa kuingia katika minada mpaka minada inafungwa korosho inakuwa bado zipo kwa wakulima bila kuuzwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Juma Satma inashangaza kuona kila mwaka kunakuwa na tatizo la uhaba wa magunia.
Alisema mkulima mtaji wake ni korosho hivyo anavyoshindwa kuuza korosho zake kwa sababu ya uhaba wa vifungashio vya kuhidhia korosho zao inashangaza.
"Tunaiomba serikali hasa wizara husika kuingilia kati tatizo hili la magunia kwani wakulima wengi korosho wameziweka majumbani kwao baada ya kukosa magunia ya kuwekea," alisema Satma
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi mkuu wa bodi ya korosho Tanzania(CBT) Alfred Francis alisema ni kweli Chama kikuu cha ushirika wa wakulima Mtwara-Masasi( MAMCU) kina uhaba wa magunia.
"Ni kweli Chama kikuu cha MAMCU kina uhaba wa magunia kwa ajili ya kusambaza katika chama vyake vya msingi lakini tatizo hili bado tunalishughulikia na litakwisha siku chache," alisema Francis
Alisema serikali inaendelea kushughulikia tatizo hilo na inaimani kuwa baada ya siku chache kuanzia sasa litapatiwa ufumbuzi na magunia yatapatikana.
Comments
Post a Comment