Mamluki katika Mashindano ya Michezo ya Wafanyakazi kuchukuliwa hatua

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ametangaza kuwachukulia hatua Wanamichezo wasiokuwa Wafanyakazi  maarufu kwa jina la “Mamluki” wanaoshiriki Mashindano ya Michezo kwa  Wafanyakazi inayojulikana kama SHIMUTA na SHIMIWI endapo watabainika.


Dkt.Mwakyembe amesema hayo  leo Jijini Mwanza wakati akifungua michezo ya Mashirika ya Umma  na Binafsi maarufu kwa jina la SHIMMUTA kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluh Hassan ambaye pia ndiye  mlezi wa mashindano hayo ambapo amesema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuimarisha afya za wafanyakazi,kubadilishana uzoefu pamoja na kutangaza Taasisi zao.

“Kuna hili suala la Wachezaji ambao sio wafanyakazi maarufu kwa jina la MAMLUKI kushiriki karika michezo hii,tena nakumbuka kuna kiongozi aliwahi kuwaita “viongeza nguvu bambikizi”,Hapa sio mahala pao nawataka wajiondoe mapema maana tukiwabaini wao pamoja na Taasisi zao tutawachukila hatua”alisema Waziri Mwakyembe

Mhe.Waziri Mwakyembe ameongeza kuwa wakati mwaka jana mashindano hayo yalipofanyika Jijini Dodoma  Mhe.Makamu wa Rais Mama Samia hakuridhishwa na idadi ya washiriki kutokana na Idadi ya Makampuni na Mashirika yaliyopo nchini,hivyo kuagiza mkutano ufanyike kujua sababu na kuzipatia majibu ambapo  maazimio yameleta matunda kwani mashindano ya mwaka huu idadi imeongezeka kutoka 26 hadi 46.


Hata hivyo Mhe.Waziri amewataka waamuzi  wa mashindano hayo kuchezesha michezo hiyo kwa haki na kufuata sheria zote za michezo  na atakayesababisha vurugu au masononeko atawajibishwa kupitia kiapo alichoapa leo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMMUTA Bw.Khamis Mkanachi amesema kuwa Menejimenti za Taasisi za Umma pamoja na Makampuni binafsi zinatakiwa kuelewa kwamba wafanyakazi wao wanatakiwa kufanya michezo mbalimbali ili kuimarisha afya zao kwa ajili ya kuongeza ufanisi wanapokuwa kazini,hivyo ni wajibu wa kila Taasisi na mashirika kuona haja ya  kutenga siku ya kufanya michezo.

“Michezo hii inafanyika kwa mwaka mara moja ni vyema viongozi wa Taasisi na Mashirika binafsi kuona umuhimu huo na kuwapa wafanyakazi wao muda wa kushiriki michezo hiyo inayoleta ari katika kufanya kazi” aliongeza Bw.Mkanachi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt.Fillis Nyimbi amesema Jiji la Mwanza hususan Wilaya ya nyamagana imeshukuru ujio wa mashindano hayo kwakua itaongeza kipato kwa wenyeji kutokana ongezeko la watu waliokuja kwa ajili ya mashindano hayo ambapo pia amewahakikishia amani na usalama.

Vilevile mwanamichezo Eliud Felix kutoka timu ya Jiji la Mwanza amesema michezo hiyo imewasaidia kujuana pamoja na kubadilishana uzoefu wa majukumu ya kila mmoja katika taasisi yake na kupendekeza iendelee kufanyika kila mwaka.

Mashindano hayo yalianza rasmi tarehe 27/11/2019 na yanatarajiwa kumalizika Desemba mosi 2019 ambapo jumla ya Mashirika na Taasisi 46 zimeshiriki ikiwemo wenyeji Ofisi ya Mkoa wa Mwanza,Chuo Kikuu Dodoma,Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na nyingine.

Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato