Tanzania kuanzisha kituo cha Kimahakama na usuluhishi wa migogoro ya Kimataifa
Tanzania na Taasisi ya ushauri wa kisheria ya Afrika (ALSF) iliyoko chini ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zimekubaliana kuandaa mkakati maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo maalum na ya haraka ya msaada wa kisheria kwa Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali (DPP) hususani katika kusimamia mashauri katika mahakama na mabaraza ya usuluhishi ya Tanzania na ya Kimataifa katika maeneo ya madini, biashara na usuluhishi na makampuni ya Kimataifa pamoja na mafuta na gesi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo mara baada ya majadiliano na Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya ushauri wa kisheria ya Afrika (ALSF) Bwana Stephen Karangizi mazungumzo yaliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Abidjan Nchini Ivory Coast.
Prof. Kabudi amesema kuwa lengo la majadiliano hayo ni kuisaidia Tanzania kuweka mikakati kuimarisha sekta ya Sheria ikiwa ni pamoja na kuiongezea uwezo ofisi ya mwanasheria mkuu wa Tanzania hasa baada ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa ya muundo mpya wa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ili kuiwezesha kutoa ushauri wa kina na wa kitaalam kwa serikali lakini pia kusimamia mashauri katika mahakama na mabaraza ya usuluhishi ya Tanzania na ya Kimataifa.
Ameongeza kuwa maombi ya Tanzania kwa taasisi hiyo kwa ajili ya kuisaidia ofisi ya mwanasheria na wakili mkuu wa serikali yamekamilika na kinachosubiriwa hivi sasa ni kuwasilisha maombi hayo kwa kikao cha bodi ili utekelezaji uanze.
Ameongeza kuwa eneo jingine ambalo Tanzania inahitaji msaada kutoka kwa Tanzania na Taasisi ya ushauri wa kisheria ya Afrika (ALSF) iliyoko chini ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ni kuhusu kuisaidia Tanzania katika hatua iliyoichukua ya kutunga sheria mpya ya usuluhishi wa migogoro ya kimataifa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo kipya cha kusimamia usuluhishi wa migogoro.
Katika eneo hilo Taasisi ya ushauri wa kisheria ya Afrika (ALSF) iliyoko chini ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itatoa wataalamu kusaidia Tanzania kupitia miswaada ambayo imeandaliwa na serikali pia kuandaa andiko la namna kituo hicho kitawekwa Tanzania na kukidhi matakwa ya kimataifa.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya ushauri wa kisheria ya Afrika Bw Stephen Karangizi amesema wamepokea ombi hilo na kwamba wanasubiri maamuzi ya kikao cha bodi ili kuweza kuanda program maalum kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali.
Ameongeza kuwa nchi nyingi za Kiafrika zimeshindwa katika usuluhishi wa migogoro hususani ya kibiashara,madini,mafuta na gesi na maeneo mengine na kuongeza kuwa suala hilo linapaswa kuwekewa mkakati maalum na kutekelezwa kwa haraka ili kuepuka makosa yaliyokwisha kufanywa katika siku zilizopita.
Taasisi hiyo ya ushauri wa kisheria ya Afrika (ALSF) iliyo chini ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilianzishwa kutokana na ombi la Mawaziri wa fedha kutoka Afrika kwa lengo la kuzisaidia Nchi za Afrika kujijengea uwezo katika masuala ya kisheria hususani katika madini,mafuta na gesi pamoja na madeni ili kuziwezesha nchi za Kiafrika kuwa na uwanda sawa wa majadiliano katika ngazi za Kimataifa kuhusu masuala ya kisheria yanahusu biashara na makampuni ya Kimataifa.
Comments
Post a Comment