RC Mtwara atoa neno kwa sekta binafsi kuhusu Miradi ya REA
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ametoa wito kwa sekta binafsi nchini kujitathmini na kufanya kazi kwa uadilifu ili kuonesha mchango wao katika kujenga nchi, hususan kupitia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Byakanwa alitoa wito huo, wakati akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Nishati Vijijini (REB), uliomtembelea ofisini kwake, ukiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani humo.
Mkuu huyo wa Mkoa amelazimika kutoa wito huo kutokana na kutoridhishwa kwake na kasi ya mkandarasi anayetekeleza mradi husika mkoani Mtwara, ambaye ni muunganiko (JV) wa kampuni za Radi Services Ltd, Njarita Contractors Ltd & Aguila Contractors Ltd.
“Nchi hii haijengwi na watumishi wa umma peke yao; Sekta binafsi nao wana hisa kwenye nchi hii, kwahiyo wasilenge kupata faida tu bali pia waoneshe mchango wao katika kujenga nchi yetu kwa kukamilisha miradi hii kwa wakati na kiwango kinachoendana na thamani ya pesa iliyotolewa,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi, Byakanwa alieleza kuwa kumekuwepo na malalamiko kutoka sekta binafsi kwamba serikali haiwashirikishi katika kutekeleza miradi mbalimbali. “Sasa wamepata nafasi ya kushiriki kwenye miradi ya REA lakini baadhi yao wameshindwa kutekeleza kwa viwango na muda stahiki.”
Mkuu huyo wa Mkoa aliipongeza Bodi ya REA kwa azimio lao la kutoa vyeti vya utambuzi kwa wakandarasi wa miradi husika watakaofanya vizuri lakini pia aliishauri Bodi hiyo kuwabainisha wale ambao utendaji wao ni wa kusuasua ili jamii ndani na nje ya nchi iwatambue na kuwaepuka.
Alisema kuwa, kitendo cha kuwatangaza waliofanya vizuri kitawasaidia wahusika kwa namna mbalimbali ikiwemo kuaminiwa na kupewa kazi na kampuni za wawekezaji wakubwa kutoka nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Byakanwa aliipongeza Bodi ya REA kuamua kufanya ziara hiyo kwani itawawezesha kujionea wenyewe hali halisi ya utekelezaji wa miradi husika badala ya kukaa ofisini na kusubiri wapelekewe ripoti.
Aidha, aliongeza kuwa, REA wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha miradi ya umeme vijijini inatekelezwa kwani wananchi wana hamu ya kupata umeme na pia wana uelewa kuhusu faida zinazopatikana kutokana na uwepo wa nishati hiyo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe husika, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi hiyo, Mhandisi Styden Rwebangila, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Bodi imejipanga kuhakikisha wakandarasi wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati uliopangwa na kwa viwango stahiki.
Baada ya kukutana na Mkuu wa Mkoa, Bodi husika ilitembelea maeneo kadhaa kunakotekelezwa mradi ikiwemo wilaya za Nanyumbu na Masasi.
Comments
Post a Comment