Mimi sikuajiriwa na mashabiki wa Yanga - Mwinyi Zahera
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema kuwa hawezi kuwasikiliza mashabiki wanachokisema kwa sasa baada ya kufungwa na Pyramids FC bali anawasiliana na uongozi ambao ulimpa mkataba.
Hayo yamekuja kufuatia mashabiki wa klabu hiyo kutoa malalamiko yao wakimtaka Zahera kuondoka kutokana na matatizo wanayosema yamekithiri kwenye kikosi ikiwemo kushindwa kupanga vizuri kikosi cha kwanza pamoja na mbinu.
“Mimi sikuajiriwa na mashabiki wa Yanga bali nilisaini mkataba na viongozi, kwahiyo siku viongozi wakinitaka kiwaachie timu nitafanya hivyo, sitokwenda mazoezini”, amesema Zahera.
“Nina uzoefu mkubwa ila hapa Afrika, mashabiki wanakasirika. Hakuna mchezaji yoyote wa Yanga anayeweza kucheza Pyramids FC na lingine ni kwamba wakati tunasajili wachezaji, hatukusajili kwa ajili ya Klabu Bingwa Afrika ila tulisajili kwa ajili ya ligi”, ameongeza.
Aidha, Zahera amesema kuwa mashabiki hawapaswi kumlaumu yeye kwa matokeo ya Klabu Bingwa kwani kikosi chake kiliandaliwa kwa ajili ya ligi kuu, ambako hawapo katika nafasi mbaya mpaka sasa, wakiwa wamecheza mechi chache.
Yanga inatarajia kusafiri hadi nchini Misri kuvaana na Pyramids katika mchezo wa marudio utakaopigwa wikiendi hii, ikiwa nyuma kwa kufungwa mabao 2-1.
Comments
Post a Comment