Madiwani Tanzania waagizwa kutoa Majina ya Mitaa
Serikali imewataka madiwani wote nchi nzima kutoa majina ya mitaa ili kufanikisha utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu umuhimu na manufaa ya kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi kwa madiwani, viongozi wa Serikali na watendaji mbali mbali wa Mkoa wa Kigoma yaliyofanyika wilayani Kibondo yaliyotolewa na wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
“Madiwani tupeni majina ya mitaa ili vifurushi, barua na vipeto viwe vinakwenda moja kwa moja kwa wananchi, tufanye biashara mtandao na kuimarisha ulinzi na usalama,” amesema Nditiye
Ameongeza kuwa biashara mtandao ni nzuri, tunataka kifurushi cha mtu kiletwe anapoishi na tayari nchi nzima kata zote zina postikodi, madiwani tupeni majina ya mitaa ili tuweke vibao na namba za nyumba ili wananchi watambulike
“Unaweza kupata postikodi ya kata au wadi yako kupitia simu yako ya mkononi kwa kupiga *152*00# kisha chagua 3 (ajira na utambuzi), 3 (TCRA – Postcode) endelea kufuata maelekezo hadi kupata postikodi ya kata yako”, amesema Nditiye
Amefafanua kuwa utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima unalenga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na anwani yake ya mahali alipo iwe mahali pa kazi, nyumbani au ofisini ili kuwezesha mwananchi kuhudumiwa kwa urahisi.
Ametoa rai kwa madiwani wote nchi nzima kutoa majina ya mitaa ili Wizara iweze kuweka nguzo zenye majina ya barabara na namba za nyumba au majengo katika maeneo yao kwa kuwa tayari kata zote nchi nzima zina postikodi
Ameeleza kuwa kuna maneno yamezoeleka kuwa Dunia ni kama Kijiji, ili dunia iweze kuwa kijiji kunategemea uwepo wa mfumo wa utambuzi wa makazi na wakazi kwa ajili ya kurahisisha utoaji na ufikishaji wa huduma kwa wananchi ambapo anwani za makazi na postikodi zinawezesha utambuzi husika na nchi zilizoendelea zilishafika hatua hii na zinaendelea kunufaika na matunda ya utambuzi husika kijamii na kiuchumi
Naye Mkuu wa Kanda ya Kati wa TCRA, Antonio Manyanda wakati akitoa mafunzo hayo amesema kuwa mpango wa anwani za makazi na postikodi utaongeza ajira kutokana na fursa za kusambaza bidhaa za wateja katika maeneo yao na mahali walipo; kurahisisha biashara mtandao hivyo kukuza uchumi; kuongeza mapato ya Serikali kwa kuwa mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa mapato zitakuwa na taarifa ya mahali walipo walipa kodi au wananchi hivyo kuwezesha ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi.
Comments
Post a Comment