Waziri Bashungwa atishia kujiuzulu TBS isipobadilika
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ametishia kujiuzulu iwapo Shirika la Viwango nchini (TBS) halitabadili mwenendo wake katika kushughulikia kero na malalamiko ya wafanyabiashara.
Bachungwa aliyasema hayo mjini Makambako Mkoani Njombe wakati alipokutana na wafanyabiashara kutoka mikoa saba nchini kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya biashara.
Katika mkutano huo uliotoka na maazimio ya kuiomba serikali kupunguza utitiri wa kodi, tozo na leseni kwa wafanyabiashara ili kunusuru sekta hiyo pia waziri huyo kwa mara nyingine tena aliinyooshea kidole TBS.
"TBS nimeshawaambia kwamba nitajiudhuru uwaziri kama hamtabadilika sasa kwa umri huu na haka kakibarua nataka nifanye vizuri."
"TBS ujumbe ndio huo nataka tushirikiane kuhakikisha utitiri wa kero zilizokuwepo zisizokuwa na lazima zinakwisha, ifike mahali basi hawa wakawe mashahidi kwamba kweli TBS mmebadilika," alisema.
Aliitaka TBS kubadilika ili kuendana na kasi ya serikali katika kushughulia kero na malalamiko ya wafanyabiashara kwa wakati bila ya urasimu.
Katika mkutano huo wizara nne zenye mahusiano ya karibu na wafanyabiashara zilialikwa ikiwemo ya Viwanda na Biashara, Tamisemi, Fedha na Uwekezaji.
Comments
Post a Comment