Vijana washauri kupima DNA kabla ya kuoana
Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Elineema Meda, amewashauri vijana kupima vinasaba (DNA) kabla ya kuona ili kuepuka kupata watoto wenye ugonjwa wa selimundu.
Akizungumza, Dk Meda alisema ni vema vijana kupima ili kujua kama wanachembechembe za selimundu kwani itasaidia kupunguza kasi ya ugonjwa huo.
“Ugonjwa huu wa selimundu unatokea pale ambapo wazazi wote wawili watakuwa DNA yenye chembechembe za selimundu, hapa ndio kunauwezekano wa wazazi kuzaa watoto wenye ugonjwa huo au hata kama hawana watakuwa na chembechembe za selimundu.
“Kasi ya ugonjwa wa selimundu imeongezeka katika bara la Afrika lakini ninachosema ni kuwa ugonjwa huu unaepukika kama vijana au wazazi watakapoamua kupima DNA kabla ya kuoana kwani wakishajua wanaweza kufanaya maamuzi ya kuchagua,”alieleza Dk Meda.
Kwa mujibu wa Dk Meda alisema utafiti uliofanywa na Muhimbili unaonesha kati ya watu 100 waliofanyiwa vipimo, 13 wanachembechembe za selimundu.
Alisema ikiwa vijana wanaendelea kuoana bila kupima DNA kujua kama wanachembechembe za selimundu, kuna uwezekano ugonjwa huo ukaendelea kuongezeka.
Dk Meda alipendekeza vipimo vya selimundu kufanywa kwa watoto wanaozaliwa kwani itasaidia kupata tiba mapema na kuokoa maisha yao.
“Wapo watoto wengi tu wanaopoteza maisha kutokana na kuchelewa kupata chanjo na matibabu ya ugonjwa huu, mimi natoa mapendekezo ya kuanzishwa kwa vipimo vya selimudu pindi watoto wanapozaliwa ili wakigundulika mapema wapewe chanjo na tiba haraka kama ilivyo kwa magonjwa ya surua, pepopunda, polio na mengineyo,”alisema Dk Meda.
Pia alitoa wito kwa wazazi kuwawahisha hospitali watoto wao pindi watakapoona dalili wasizozielewa na si tu kuwanunulia dawa na kuwapa.
Comments
Post a Comment