Mgonjwa wa miaka 101 awekewa kifaa Maalum cha kurekebisha mapigo ya moyo JKCI
Kwa mara ya kwanza madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamwekea mgonjwa mwenye umri wa miaka 101 kifaa maalum cha kurekebisha mapigo ya moyo ili yawe sawa (kwa jina la kitaalamu Pacemaker).
Kifaa hicho kisaidizi cha moyo huwekewa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimi 30 kwa dakika.
Akizungumza baada ya kumfanyia upasuaji mdogo na kumwekea mgonjwa kifaa hicho Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Yona Gandye alisema mara nyingi wanawawekea kifaa hicho wagonjwa wenye umri wa miaka 80 kushuka chini lakini leo hii wamevunja rekodi na na kuweka kwa mgonjwa wa umri wa miaka 101.
“Kabla ya kufanya upasuaji tulimfanyia mgonjwa uchunguzi wa kina na kugundua mfumo wake wa umeme wa moyo unahitilafu na mapigo ya moyo yapo chini ya asilimia 20 hivyo tumemuwekea kifaa ambacho kitausaidia moyo kuongeza mapigo yake na mara baada ya kumwekea kifaa hiki mapigo yake ya moyo yako vizuri kati ya asilimia 60 na 100 kwa dakika”, alisema Dkt. Gandye.
Akizungumza kwa furaha mara baada ya baba yake kuwekewa kifaa hicho Saimoni Maina alisema matatizo ya baba yake yameanza mwaka mmoja uliopita na kutibiwa katika hospitali mbalilmbali Mkoani Manyara na Arusha ambapo waligundua kuwa mapigo yake ya moyo yapo chini hivyo kumpa rufaa kwa ajili ya kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Baba alikuwa akianguka na kupoteza fahamu mara kwa mara ndipo tukaamua kumpeleka hospitalini kwa ajili ya matibabu ili kufahamu anasumbuliwa na tatizo gani, tunashukuru sana uwepo wa Taasisi hii kwani baba yetu ameweza kufanyiwa upasuaji na hali yake inaendelea vizuri kama mnavyomuona”, alisema Maina.
Kwa upande wake Mzee Benedict Maina alisema kabla ya kufanyiwa kwa upasuaji huo alikuwa akipata maumivu makali sehemu za moyo, kuanguka, kupoteza fahamu na kushindwa kutembea lakini baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali yake imebadilika na maumivu kupungua ukilinganisha na ilivyokuwa awali na anaamini siku chache zijazo atarudi katika hali yake ya kawaida.
Comments
Post a Comment