Kupatiwa chakula mashuleni, Kiwango cha ufaulu chaongezeka
Na. Clavery Christian Kagera
Halmashauri ya wilaya Biharamulo mkoani Kagera imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa madarasa ya awali, darasa la nne, na darasa la saba baada ya kuanza kuwapatia huduma ya uji na chakula mashuleni.
Hayo yamesemwa na mh, Samweli Kalimanzira mwenyekiti wa kamati ya elimu, maji na afya katika kikao cha robo ya nne ya mwaka cha balaza la madiwani wilayani humo ambapo amesema kuwa ufaulu wa wanafunzi mashuleni umeongezeka kutokana na shule nyingi za wilaya hiyo kuanza kutekeleza maamuzi ya kamati hiyo ya kuwapatia uji na chakula wanafinzi mashuleni ili kuwaondolea hali ya kuwa darasani wanawaza wataondoka saa ngapi kwenda nyumbani kula kutokana na njaa wanayokuwa nayo.
Kamati hiyo imeshauri kuwa shule kumi (10) ambazo zimebaki bila kuwa na huduma ya uji wala chakula shuleni wazazi na walezi waendelee kuhamasishwa na watumishi wakishirikiana na madiwani ili shule hizo ziweze kutoa huduma hiyo kwa wanafunzi bila kuchelewa.
Aidha kamati imependekeza kuwa uhamasishaji ufanyike wa mashamba darasa mashuleni ili kuondoa kero ya uji na vyakula mashuleni.
Sambamba na hayo kamati pia ilishauri kuwa adhabu ya viboko mashuleni inasababisha utoro hivyo mkakati uwekwe wa kupunguza viboko mashuleni.
Aidha maafisa elimu watoe maelekezo ya utoaji wa adhabu kwa kufuata sheria na kanuni za adhabu kwa mwanafunzi. Kamati ilimaliza kwa kushauri kuwa katika ugawaji wa fedha za maendeleo katika shule ziwe zinaangaliwa pia shule shikizi ili kuweza kuziboresha na hatimaye zikaanza kujiendesha.
Comments
Post a Comment