Wanaofanya shughuli kwenye hifadhi za wanyama watakiwa kuhama
Wananchi wenye makazi na wanaofanya shughuli zao kwenye hifadhi za wanyama wilayani Songwe, wametakiwa kuhama kutoka maeneo hayo kwa kuwa si salama na yanahatarisha maisha yao kutokana na uwapo wa wanyama wakali.
Kwa mujibu wa ofisa maliasili kata ya Kapalala, wilayani Songwe, Benard Nenje, kumekuwapo na matukio mengi ya wakazi wa maeneo yaliyo jirani na hifadhi kushambuliwa na wanyama sambamba na kuharibiwa mali zao ikiwamo mazao shambani.
Akizungumza, Nenje alisema kwa mwaka jana pekee, wananchi 24 walipata madhara ya kuvamiwa na wanyama, ambapo kati yao 22 wanatokea kata ya Gua na wawili kata ya Ngwala ambao serikali ililazimika kuwalipa fidia kutokana na mazao yao kuliwa na tembo.
Alisema kwa mwaka huu wananchi 30 wanatakiwa kulipwa fidia kutokana na tembo kula mazao yao na wengine kujeruhiwa na simba na fisi.
Ofisa huyo alisema asilimia kubwa ya wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi wanakuwa hawaelewi madhara yake hivyo kujikuta wakijenga makazi na kujishughulisha na kilimo bila kuujulisha uongozi wa kijiji pamoja na kata ili kupata utaratibu.
Watu hao wamekuwa wakijeruhiwa na wanyama wakali wakiwamo simba pamoja na mazao yao kuliwa na tembo jambo linaloigharimu serikali kuwalipa fidia kutokana na kosa walilofanya wenyewe," alisema.
Comments
Post a Comment