Makusanyo ya kodi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya jumla ya TZS 15.9 trilioni kati ya lengo la TZS 18 trilion kwa mwaka wa Fedha 2018/19 kuanzia tarehe 1 Julai 2018 hadi 30 Juni 2019.
Aidha katika robo ya nne ya mwaka huo wa fedha yaani, mwezi Machi hadi Juni 2019, TRA ilikusanya TZS 1.1 trilioni, TZS 1.2 trilioni, na TZS 1.5 trilioni kwa mwezi Aprili, Mei, na Juni, mtawalia. Kwa namna ya kipekee kabisa, TRA inawashukuru walipakodi na wananchi wote kwa ujumla kwa ushirikiano.
Ikumbukwe kwamba, katika mwaka huo wa fedha, Serikali ilianzisha Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) ambao utekelezaji wake umefanyika kwa awamu mbili (2). Awamu ya kwanza, ilihusisha bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia na aina zote za vileo. Awamu hii ya kwanza iliyoanza kutekelezwa tarehe 15 Januari 2019 imeendelea vizuri na maandalizi ya awamu ya pili ya utekelezaji wa ETS inayojumuisha bidhaa za vinywaji baridi, maji, juisi, na CD/DVDs yamekamilika.
Hivo mfumo huu wa ETS kwa awamu hii ya pili, unatarajiwa kuanza kazi rasmi tarehe 1 Agosti, 2019.
Lengo kuu la kubandika stempu hizi za kielektroniki ni kuongeza usimamizi na ufanisi wa ukusanyaji wa Ushuru wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kupata taarifa sahihi za uzalishaji viwandani ili kukusanya mapato stahiki.
Ni matumaini ya TRA kuwa, wazalishaji, waingizaji, wasambazaji, wauzaji wote wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa pamoja, na umma kwa ujumla wataendelea kutoa ushirikiano kwa TRA ili kufanikisha utekelezaji wa mfumo huu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Comments
Post a Comment