Walimu wa masomo ya Hisabati na Sayansi kukuza ufaulu nchini


Walimu wa masomo ya  Hisabati  na Sayansi nchini wametajwa kuwa chachu ya kuendelea kukuza kiwango cha ufaulu katika masomo hayo na hivyo kuchochea ujenzi wa dhana ya uchumi wa viwanda.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa mwaka wa chama cha walimu wa Hisabati na Sayansi   Jijini Dodoma Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera Uratibu na Uwekezaji) Bi Dorothy Mwaluko amesema kuwa walimu wa masomo hayo wamekuwa wakifanya kazi kubwa yakuwaandaa vyema wanafunzi wanaochukua michepuo ya sayansi na hivyo kuchochea ufaulu kuongezeka.

“ Nawapongeza na kuwataka muongeze juhudi katika kuhakikisha kuwa tunasaidia katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwani unategekea wataalamu wa Hisabati na Sayansi ili azma hii ya Serikali ya Awamu ya Tano iweze kutimia kwa wakati” Alisisitiza Bi Mwaluko.

Akifafanua amesema kuwa walimu wa masomo hayo wamekuwa wakijitoa kwa dhati kutekeleza majukumu yao ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupenda masomo ya Sayansi na Hisabati na hatimaye kukuza kiwango cha ufaulu.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mkutano huo ambaye pia ni mwanachama wa chama cha walimu wa Hisabati na Sayansi Bi Masika Lazaro amesema kuwa changamoto kubwa kwa walimu hao ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi wanayapenda na wanaongeza jitihada katika kujifunza.

Aliongeza kuwa kama chama wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali za kuwawezesha wanafunzi kujifunza na kupenda masomo hayo hali inayoongeza ufaulu .

Chama cha walimu wa Hisabati na Sayansi kimekuwa na manufaa makubwa kwa walimu wa masomo hayo kwa kuendesha mafunzo yakuwajengea uwezo zaidi wanachama wake kote nchini ili kukuza masomo hayo.

Mkutano wa chama cha  Walimu wa Hisabati na Sayansi umefanyika Jijini Dodoma ukiwa ni mkutano wa kwanza wa chama hicho tangu kilipoanzishwa kikiwa na dhamira ya kukuza na kuendeleza masomo hayo hapa nchini ili kutoa mchango unaostahili katika uchumi.

Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato