Mtambo wa Megawati 300 kutengenezwa Mtwara
Na Omary Mngindo, Mkuranga
SERIKALI imeeleza kuwa ina mpango wa kutengeneza mtambo mkubwa utaozalisha Megawati 300 za umeme, kisha kuusafirisha kutoka mkoani Mtwara kwenda Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu ameyasema hayo alipozungumza na wananchi wa Kijiji cha Njopeka, Kata ya Mjawa wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, akiwa kijijini hapo mwishoni mwa wiki, ambapo alisema hatua hiyo inalenga kuboresha huduma ya umeme.
Aidha alisema kuwa serikali imefanya tathmini ya fidia kwa wananchi wa maeneo ya Rufiji, Mkuranga na Dar es Salaam ambao wamepitiwa na bomba la gesi na nguzo za umeme, huku akiombaradhi kuchelewa kulipwa fidia, na kwamba zoezi hilo linataraji kuanza Julai mwaka huu.
"Malipo yataanza mwezi Julai kwa wakazi waishio Mkoa wa Dar es Salaam, baada ya hapo zoezi litaendelea tena kuanzia mwezi wa nane mpaka wa kumi na mbili mwaka huu kwa wakazi wa maeneo ya Mkuranga, niwaomberadhi kwa kuchelewa fidia hizo" alisema Mgalu.
Aidha Mgalu amewataka mafundi shirika la umeme Kanda ya Rufiji kuweka kambi katika eneo la Njopeka, ili kuhakikisha wanasambaza umeme katika nyumba za wananchi sanjali na kwenye kisima cha maji, lengo kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi kijijini hapo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo Alhaj Abdallah Ulega, ameelezea shukrani zake kwa serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ya usambazaji umeme jimboni mwake.
"Nikuondoe hofu dada yangu Mgalu, Serikali kupitia wizara yenu ya Nishati mmefanyakazi kubwa sana ya kusambaza umeme katika vijiji jimboni kwangu, nitumie fursa hii kuishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa namna inavyosimamia usambazaji wa nishati hii," alisema Ulega.
Nae Mwenyekiti wa Kijijini cha Njopeka Mwarami Mketo alisema kuwa tangu kijiji hicho kianzishwe pamoja na.kupitiwa na umeme mkubwa ndio kwanza wanaonja radha ya umeme.
Comments
Post a Comment