Biashara ya nafaka ya mtaji mdogo
Iwapo wewe ni muajiriwa na muda haukutoshi kujiingiza katika biashara kubwa zinazohitaji muda, basi amua kufanya biashara hii ya nafaka.
Wapo ambao wanaishi katika nyumba zenye nafasi ya kutosha, pia wapo ambao wana chumba kimoja na sebule na hawana mahali pa kuhifadhi magunia kadhaa ya nafaka.
Ila iwapo una vyumba viwili basi angalia namna ya kugawa nafasi hiyo uweze kuweka hata angalau gunia 20 za kilo hamsini hamsini kwa kuanzia ili utapopata faida ya msimu huu uweze kujiwekea malengo ya kupangisha chumba kimoja cha ziada.
Kwa kawaida nafaka zote huwa bei ndogo wakati zinapovunwa na bei hupanda pole pole kadri muda unavyoenda. Hivyo hakuna siku utapata hasara kwa kuhifadhi nafaka zilizovunwa endapo utafuata taratibu za uhifadhi ili nafaka zisiharibiwe na wadudu ama panya.
Hebu tuchukulie kwa mfano, mwezi mmoja baada ya watu kuvuna mahindi na maharage ukaamua kununua kilo 500 za mahindi na kilo 500 za maharage. Ukazihifadhi katika magunia ya kilo hamsini hamsini. Utakuwa na gunia kumi za mahindi na gunia kumi za maharage. Endapo utanunua mwezi mmoja baada ya mavuno kuna uwezekano mkubwa ukapata gunia la kilo mia za mahindi kwa 36,000/= na gunia la kilo mia la maharage kwa 50,000/=.
Kilo 500 za mahindi itakuwa sawa na 180,000/= na kilo 500 za maharage itakuwa sawa na 250,000/=. Jumla ni 430,000/=. Hii ni pesa ambayo unapaswa kuilimbikiza ili kumlipa kodi mwenye nyumba na haitoshi kulipia miezi sita kwa vyumba viwili. Sasa endapo utaamua kuitumia hii pesa kuzalishia ili faida utayopata ndo ulipe kodi basi utakuwa hutumii mshahara wako kulipa kodi ya nyumba. Hapo utakuwa umepunguza ukali wa maisha kwa namna ya kipekee.
Ukiona msimu wa mavuno umefika hebu wasiliana nao kule kijijini kila siku wakutumie japo kilo mia kwenye basi la abiria. Baada ya wiki mbili utakuwa ushapata hizo kilo 500za mahindi na 500 za maharage.
Tena baada ya miezi mitatu usihangaike kutafuta soko, pakia kwenye basi lile lile uwaambie huko kijijiji wapokee na wauze kwa debe la mahindi 25,000/= na debe la maharage 34,000/=. Kumbuka gunia ni debe tano. Hivyo basi kila gunia la mahindi ulilolinunua kwa 36,000/= utaliuza mara tano ya bei ulonunulia na utajipatia 125,000/= kwa gunia.
Endapo utauza magunia matano uliyonayo kwa bei hii basi utajipatia takriban 625,000/= kutoka katika mahindi pekee. Kutoka katika maharage, utajipatia 170,000/= kwa gunia moja. Endapo utauza kwa bei hii magunia yote matano utajipati 850,000/=. Jumla ya mahindi na maharage ni 1,475,000/= kutoka katika ile 430,000/= ya awali. Hapa utakuwa umetumia takriban 300,000/= katika usafiri na uhifadhi.
Sasa hebu tuangalie namna ya kuhifadhi mahindi na maharage katika magunia. Kabla ya kuweka mahindi kwenye magunia inabidi kuchukua tahadhari ya kuzuia uharibifu utokanao na wadudu na panya.
Mahindi na maharage yanapaswa kuchanganywa na viua dudu. Viua dudu vinavyopendekezwa Tanzania ni Actelic Super Dust. Actelic Super Dust hupatikana maduka ya pembejeo. Kwa kawaida gramu 100 za kiuwadudu hiki huchanganywa na kilo 100 za mahindi/maharage.
Comments
Post a Comment