Naibu Waziri, Ikupa awaomba wadau kuwasaidia Walemavu


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau kuendelea kutoa msaada wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa hili ni hitaji endelevu kwa watu hao.

Ikupa ameyasema hayo Februari 27, 2019 wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali wilayani Busega mkoani Simiyu wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.

Amewashukuru viongozi wa Wilaya ya Busega kwa namna inavyowasaidia watu wenye ulemavu katika kuwapatia vifaa saidizi huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuwatafutia na kuwapatia watu wenye ulemavu vifaa hivyo kwa kadri vitakavyopatikana.

"Napenda kuwashukuru viongozi wa Busega kwa namna wanavyowasaidia watu wenye ulemavu kupata vifaa saidizi kama fimbo nyeupe kwa wasioona, baiskeli na viungo bandia kwa walemavu wa viungo, mafuta kwa wenye ualbino, lakini niwaombe wadau waendelee kuwasaidia kwa kuwa hili ni hitaji endelevu katika kuishi kwao." alisema Ikupa.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amesisitiza Kamati za watu wenye ulemavu kupewa miongozo ya namna ya kuziendesha kamati hizo, ili ziweze kutimiza majukumu yake ipasavyo na kuzitaka kutoa taarifa kuhusu fursa na masuala mbalimbali yanayowahusu walemavu katika maeneo yao.

Vile vile Ikupa amesema Serikali inatarajia kuanzisha mfuko wa watu wenye ulemavu ambao utakuwa ukishughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku kwa vyama vya walemavu.

Akitoa taarifa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, amesema Serikali wilayani imetoa baiskeli 17 kwa watu wenye ulemavu wa viungo, zaidi ya fimbo nyeupe 50 kwa wasioona, mafuta kwa watu wenye ualbino na Halmashauri imeandaa mpango maalum wa Mfuko wa Bima ya Afya(CHF) iliyoboreshwa kwa ajili ya huduma za afya kwa walemavu.

Kwa upande wao watu wenye ulemavu wameiomba Serikali na wadau kuendelea kuwapa msaada wa vifaa saidizi , kupewa elimu ya kuunda vikundi na kuandaa maandiko ya miradi na kutoa semina elekezi kwa kamati za watu wenye ulemavu.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Stella Ikupa amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Simiyu Febrauari 27, 2019 ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na  viongozi wa serikali, watu wenye ulemavu na kukagua mradi wa kitalu nyumba katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu.

Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato