IGP Sirro atoa neno kwa Wafanyakazi na wananchi wanaozunguka Mradi wa SGR
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro, amewataka wafanyakazi na wananchi wanaozunguka Mradi wa Reli ya Kisasa SGR kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu badala yake watoe ushirikiano kwa Kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga mradi huo unaotumia fedha za ndani za Watanzania.
Akizungumza wakati alipofanya ziara kwenye mradi huo kutoka kituo cha Ilala hadi Kilosa mkoani Morogoro, IGP Sirro amesema kuwa, kila mmoja anayo nafasi ya kufanya ili kuhakikisha mradi huo unamalizika kwa haraka na katika muda uliopangwa bila kuwa na vikwazo.
Aidha, IGP Sirro amesema kuwa, Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote hata pale mradi huo utakapokamilika na kukabidhiwa kwa serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amesema kuwa ziara ya Mkuu wa Jeshi la Polisi imewaongezea ari ya kufanyakazi saa 24 bila kuwa na hofu ya kiusalama.
Comments
Post a Comment