Hatma rufaa ya Mbowe na Matiko kujulikana leo
Mahakama ya Rufani leo inatarajia kutoa uamuzi wa rufaa iliyokatwa na DPP dhidi ya Wabunge Freeman Mbowe na Esther Matiko. Uamuzi huo huenda ukairuhusu Mahakama Kuu kuendelea kusikiliza rufaa iliyokatwa na washtakiwa hao baada ya kufutiwa dhamana, au ikatupilia mbali rufaa hiyo.
Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.
Wawili hao walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kwa Jaji Sam Rumanyika.
Hata hivyo, baada ya mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.
Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu.
Rufaa ya (DPP) dhidi ya Mbowe na Matiko ilisikilizwa chini ya jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Stella Mgasha, Mwanaisha Kwariko na Gerald Ndika.
Comments
Post a Comment