TBA watakiwa kukamilisha miradi kwa wakati
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (rtd) Nicodemus Elias Mwangela amewataka Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) kukamilisha miradi ya ujenzi wanayo pewa ndani ya muda wa makubaliano ya mikataba.
RC Mwangela ameyasema hayo jana wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ya ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Mkoa na ya Katibu Tawala Mkoa kati ya TBA na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe.
“TBA mna sifa nzuri ya kujenga majengo ya serikali kwa kuzingatia ubora unaotakiwa na kwa gharama nafuu lakini kuna wakati kunakuwa na kusita katika kuwapa kazi kutokana na historia yenu ya kuchelewesha kukamilisha miradi mnayopewa ya ujenzi”, ameeleza Brig. Jen. (rtd) Mwangela.
Ameongeza kuwa TBA wamechelewesha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na ujenzi wa Hospitali ya Mji wa Tunduma hivyo ucheleweshaji huo usirudie katika mikataba hiyo miwili waliyopewa kwani hatasita kuvunja mikataba hiyo endapo wataonyesha ucheleweshaji.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Z. Kafulila ameishukuru serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuupatia Mkoa wa Songwe kiasi cha shilingi bilioni 26.8 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali mkoani hapa.
Kafulila amesema serikali imekuwa ikitoa fedha za miradi mbalimbali lakini kasi ya utoaji wa fedha na matumizi ya fedha hizo kwenye miradi husika imekuwa haiendani na hivyo kusababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Songwe Mhandisi Fidelis Cosmas ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwa amini na kuwapa miradi hiyo miwili yenye thamani ya shilingi bilioni moja na kuahidi kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Comments
Post a Comment