Adakwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua Mama yake mzazi kwa Kisu


Mkazi wa Kijiji cha Moleti Wilaya ya Kongwa Peter Mgomba (26), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kumuua mama yake mzazi kwa kumchoma kisu tumboni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari, jiijini hapo jana.

Kamanda Muroto alisema tukio hilo lilitokea Desemba 29, katika Kijiji cha Moleti, Tarafa Mlali, Wilaya ya Kongwa.

Alisema tukio la mauaji linadaiwa kufanyika wakati Mgomba alipomchoma kisu tumboni mama yake mzazi, Anita Mgomba (61) na kusababisha kifo.

Alisema chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika, lakini wanaendelea na uchunguzi na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Hata hivyo, Kamanda Muroto alisema mtuhumiwa anasadikiwa kuwa ni mgonjwa wa tatizo la akili na baada ya kufanya tukio alitoroka, lakini jeshi hilo lilimtafuta na kumtia nguvuni.

Alisema siku ya tukio, Anita alijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini, lakini akiwa kwenye matibabu Desemba 30, alifariki dunia.

Wakati huo huo, Kamanda Muroto alisema, Polisi inawashikilia watu wanne kwa kudaiwa kuiba saruji mifuko 50 katika eneo la ujenzi wa majengo ya serikali Chamwino Ikulu mkoani Dodoma.

Alisema watuhumiwa walikamatwa wakiwa wamepakia mifuko hiyo ya saruji kwenye lori.

Kamanda Muroto alisema watuhumiwa wanasadikiwa kuvunja stoo na kufanikiwa kuiba mifuko hiyo 50 ya saruji kwa lengo la kwenda kuiuza.



Comments

Popular posts from this blog

Mwenyekiti aishauri Serikali kuhalalisha uchangudoa ili kujipatia mapato